1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini, Mali ndani ya robo fainali ya AFCON

31 Januari 2024

Morocco wamekuwa miamba ya karibuni kabisa kuondolewa katika Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON lililojaa maajabu. Morocco walifungwa 2 – 0 na Afrika Kusini jana usiku, wakati pia Mali walijikatia tiketi ya robo fainali.

Afrika Kusini waliwazidi nguvu Morocco waliofika nusu fainali ya Kombe la Dunia
Bafana Bafana sasa watakutana na Cape Verde katika robo fainali Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Evidence Makgopa na Teboho Mokoena walifungia Bafana Bafana katika kipindi cha pili, waliodhihirisha kwa mara nyingine kuwa timu sumbufu kwa Atlas Lions, ambayo Achraf Hakimi alikosa penalti.

Soma pia: Cote d'Ivoire, Cape Verde zaingia robo fainali AFCON

Tangu kuwa timu ya kwanza ya Afrika kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar miaka miwili iliyopita, Morocco wameshindwa mechi mbili kati ya 13, na vichapo hivyo viwili vilitoka kwa Afrika Kusini.

Soma pia: Kongo, Guinea zatinga robo fainali ya AFCON

Matokeo hayo ya kushtusha ya hatua ya 16 za mwisho katika mji wa pwani ya Cote d'Ivoire wa San-Pedro yamejiri baada ya Mali kuizidi nguvu Burkina Faso kwa kuilaza 2 – 1 katika mji wa Korhogo huku Lassine Sinayoko akifunga bao lililokuwa na umuhimu mkubwa.

Evidence Makgopa aliiweka Afrika Kusini kifua mbelePicha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Vigogo waangushwa

Morocco wanajiunga na mabingwa watetezi Senegal, Tunisia, Algeria, Cameroon na Burkina Faso kama timu zinazoorodheshwa katika nafasi 10 za juu barani Afrika kwa viwango vya FIFA ambazo zimefungasha virago mapema.

Soma pia: Magoli 2 ya Lookman dhidi ya Kamerun yaipeleka Nigeria robo fainali

Afrika Kusini watakwaruzana na Cape Verde mjini Yamoussoukro Jumamosi baada ya wenyeji Cote d'Ivoire na Mali kukabana koo mjini Bouake.

Katika mechi nyingine za robo fainali, Nigeria yake Victor Osimhen itashuka dimbani na Angola, wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakutana na Guinea Ijumaa.

Afrika Kusini, Cote d'Ivoire, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni mabingwa wa zamani wakati washindani hao wengine wanne wanatumai kubeba ubingwa kwa mara ya kwanza.

Licha ya kuwa miamba ya Afrika kwa miongo mingi, Morocco mara kwa mara wameshindwa kufanya vyema katika AFCON tangu walipobeba taji katika ardhi ya nyumbani miaka 48 iliyopita.

Kocha wa Morocco akubali lawama

Morocco walibaki kujutia nafasi nyingi walizopotezaPicha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Kocha wa Walid Regragui amesema baada ya mechi kuwa wamesikitishwa sana kwa sababu walikuwa na malengo ya kushinda taji hilo. Kwamba hawakutarajia kuondoka mapema katika mashindano hayo lakini Kombe hilo ni gumu mno kushinda. Amesema yeye ndiye anapaswa kulaumiwa kwa kichapo hicho.

Simba wa Atlas ambao walitengeneza nafasi nyingi, waliduwazwa wakati Themba Zwane alimuandalia pasi murwa Makgopa kufunga. Walipambana na kupata penalti katika dakika ya 82 lakini Achraf Hakimi akashindwa kufunga maana shuti lake liligonga chum ana kupaa juu. Aidha Sofyan Amrabat alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi, na Mokoean akapigilia msumari wa mwisho kwa kufunga freekick safi sana. Katika mechi ya mapema, Sinayoko alifunga bao lake la tatu katika mashindano haya wakati Mali ilitinga robo fainali kwa mara ya kwanza tangu 2013 kwa kuilaza Burkina Faso 2 – 1.

Beki wa Burkina Edmond Tapsoba alijifunga bao la mapema na kuiweka Mali kifua mbele mapema kipindi cha kwanza kabla ya Sinayoko kuongeza la pili punde baada ya kipindi cha pili kuanza. Nahodha Bertrand Traore alifungia Burkina Faso penalti na kuwarejesha mchezoni lakini bao la Issoufou Dayo lilifutwa kwa kuwa alikuwa ameotea.

"Ilikuwa mechi ngumu kweli dhidi ya timu nzuri. Tulihitaji kufanya kazi ya ziada lakini nna furaha hatimaye tulipata matokeo.” Alisema Sinayoko.

afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW