1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini, Urusi zaimarisha uhusiano wa kijeshi

24 Januari 2023

Waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov alikuwa Pretoria Jumatatu kwa mazungumzo na mmoja wa washirika muhimu wa Moscow barani Afrika, wakati Afrika Kusini ikijiandaa kwa mazoezi ya pamoja na Urusi na China mwezi ujao.

Südafrika Besuch Außenminister Lawrow Russland
Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Jeshi la Afrika Kusini litakuwa wenyeji wa mazoezi ya kijeshi ya pamoja na Urusi na China katika pwani yake ya mashariki kuanzia Februari 17 hadi 27.

Mazoezi hayo ya kijeshi yatafanyika sanjari na maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo tarehe 24 Februari.

Ingawa Afrika Kusini ina biashara kidogo na Moscow, inaunga mkono msimamo ambao Urusi na Chinaa zimechukua katika kupunguza kile kinachoonekana kuwa ushawishi wa Marekani katika jukwaa la kimataifa.

Kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita, chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC) kimejitanabahisha kuwa na wajibu kwa Kremlin kama shukrani kwa uungwaji mkono wa kimaadili na kijeshi katika mapambano ya Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Baerbock na Colonna wahimiza mshikamano wa Afrika dhidi ya Putin

01:34

This browser does not support the video element.

Soma pia: Urusi, Afrika Kusini zatetea mazoezi ya kijeshi na China

Na wakati huo huo, msimamo wa Afrika Kusini iliyojitangazia wa kutoegemea upande umeavunja moyo washirika wake wa magharibi, ambao wanaichukulia nchi hiyo kuwa muhimu kwa mipango yao ya kuimarisha uhusiano na Afrika.

Jumatatu waziri wa mambo ya nje na ushirkiano wa kimataifa wa Afrika Kusini Naledi Pandor alijibu ukosoaji wa mazoezi hayo ya pamoja, akisema kuandaa mazoezi kama hayo na marafiki ndiyo "mwekeleo wa asili wa uhusiano."

Sera ya kigeni ya Afrika Kusini 'lazima iunge mkono haki za binadamu'

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye amejitolea kuwa mpatanishi katika mzozo wa Ukraine, anasisitiza kuwa serikali yake haiegemei upande. Upinzani wa kisiasa na wawakilishi wengi wa mashirika ya kiraia wanapinga kauli hiyo.

Darren Bergman, mwanachama wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, anasema inazidi kudhihirika wazi kwamba serikali ya Afrika Kusini inaegemea wazi wazi upande wa Urusi.

Soma pia: Scholz aizungumzia Ukraine katika ziara yake Afrika Kusini

Mwenyekiti mtendaji wa wakfu wa Democracy Works wenye makao yake mjini Johannesburg, William Gumede, aliiambia DW kwamba msimamo wa Afrika Kusini ni hali mbali na kinyume cha katiba kwa sababu katiba ya nchi hiyo inaweka wazi kwamba sera yao ya kigeni laazima iunge mkono haki za binadamu.

Hii ni ziara ya pili ya Lavrov barani Afrika katika muda wa miezi sita, na inakuja kuelekea mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika, ambao mwaka jana uliahirishwa hadi Julai 2023 kutokana na vita nchini Ukraine.

Watu kutoka chama cha wa Ukraine nchini Afrika Kusini wakiandamana nje ya wizara ya uhusiano wa kimataifa ambako waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Naledi Pandor alikuwa akifanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov mjini Pretoria, Afrika Kusini, Januari 23, 2023.Picha: Alet Pretorius/REUTERS

Afisa wa Afrika Kusini ambaye alikataa kutajwa jina kwa sababu hakuruhusiwa kuzungumza, alisema Lavrov atazuru pia mataifa ya Eswatini, Botswana na Angola wakati wa ziara hiyo.

Ombi la Ukraine kuungwa mkono barani Afrika

Ubalozi wa Ukraine mjini Pretoria umeiomba Afrika Kusini kusaidia kuidhinisha mpango wa amani wa vipengele 10 ambao Rais Volodymyr Zelenskiy alipendekeza kwa kundi la G20 Novemba iliyopita.

Soma zaidi: Biden: Afrika inastahili dhima kubwa zaidi duniani

Zelenskiy amejaribu mara kwa mara kuimarisha uhusiano wa Ukraine na Afrika kwa mafanikio kidogo mpaka sasa.

Mataifa mengi ya Afrika yamekuwa yakisita kuchukuwa upande, kama ilivyoweka wazi wakati wa kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kusitisha uanachama wa Urusi katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Aprili iliyopita, wakati mataifa 10 kati ya 54 ya Afrika, yalipopiga kura kuunga mkono. Tisa yalipinga azimio hilo na 35 yalijizuwia au hayakuwepo.

Mwezi moja kabla, mataifa 28 tu ya Afrika yaliunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa lililotaka uondoaji mara moja na usio na masharti wa vikosi vya Urusi kutoka Ukraine. Kwa sasa Urusi ndiyo muuzaji mkuu wa silaha kwa bara la Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti ya mapitio ya taasisi ya kimataifa ya amani, usafirishaji wa silaha barani Afrika ulichangia asilimia 18 ya mauzo yote ya silaha ya Urusi katika miaka ya 2016 na 2020.

Mnamo Januari 2022, mamia ya washauri wa kijeshi wa Urusi walipelekwa nchini Mali. Kwa mujibu wa jeshi la Mali, wakandarasi kutoka kundi la kijeshi la Wagner walialikwa kuisaidia Mali kutoa mafunzo kwa vikosi vyake.

Jirani ya Mali upande wa kusini, Burkina Faso, ambayo pia ilishuhudia mapinduzi ya kijeshi Januari iliyopita, na kufuatiwa na mapinduzi ya pili mwezi Septemba, pia imejielekeza kwa Urusi baada ya kukataa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Mazoezi ya mwisho ya kijeshi kati ya Afrika Kusini, Urusi na China yalifanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini, Novemba 24, 2019.Picha: Chen Cheng/Photoshot/picture alliance

Urusi yalenga kuwa 'mtetezi wa Afrika'

Sudan, Chad, Guinea na Guinea Bissau pia zimepitia mapinduzi katika miaka ya karibuni. Na wanajeshi wengi walioko nyuma ya mapinduzi hayo wamepokea mafunzo yaliofadhiliwa na Urusi.

Kwa mujibu wa Irina Filatova, kutoka chuo cha juu cha uchumi cha mjini Moscow, Urusi inalenga kujizatiti barani Afrika kama mpatanishi ili kukabiliana na mataifa ya magharibi, na kuonesha taswira ya mtetezi wa Afrika.

Soma pia: Ukraine kuimarisha uhusiano na bara la Afrika

Kufuatia kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia na hadi kwenye miaka ya 1970, Kremlin iliunga mkono mavuguvugu ya ukombozi kote barani Afrika, wakati huo ikiuza silaha ndogo ndogo za masafa mafupi na ya kati.

Wengi walikaribisha ushawishi unaoongezeka wa Urusi barani Afrika, wakiutaja kuwa kichocheo cha uhuru wa mataifa mengi.

Uungaji huu mkono hata hivyo uliyeyuka kufuatia kuanguka kwa Jamhuri ya Kisovieti mnamo mwaka 1991.

Lakini katika miongo miwili iliyopita, viongozi wa Urusi wamejaribu kufufua uhusiano huo wa baada ya zama za uhuru.

Urusi imebakia kimya rasmi kuhusu siasa zake na Afrika. Lakini, kama anvyoona Filatoba, Moscow inategemea kampuni binafsi za kijeshi kama Wagner kuifungulia milango ya bara hilo.

Meli ya UN iliyobeba nafaka yaelekea Afrika kutoka Ukraine

01:08

This browser does not support the video element.

Mikhail Bushuev, Abu-Bakarr Jallow, Chritina Krippahl wamechangia kwenye makala hii.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW