1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Afrika Kusini yaadhimisha miaka 30 ya demokrasia

27 Aprili 2024

Afrika Kusini imeadhimisha siku ya Jumamosi (27.04.2024) miaka 30 ya demokrasia baada ya kumalizika utawala kandamizi na wa kibaguzi, ikiwa ni takriban mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi wenye ushindani mkubwa.

Mchoro wa Nelson Mandela huko Soweto
Mwanamke wa Afrika Kusini akiangalia mchoro wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Nelson Mandela huko Soweto: 07.12.2013Picha: AFP via Getty Images

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alipongeza mafanikio ya nchi hiyo chini ya uongozi wa chama chake cha African National Congress (ANC).

"Afrika Kusini leo ipo mahali pazuri zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 30 iliyopita," Ramaphosa alisema katika hotuba yake ya kuadhimisha "Siku ya Uhuru" katika Majengo ya Muungano mjini Pretoria ambayo ndio makao makuu ya serikali.

Ramaphosa mwenye umri wa miaka 71 ametumia fursa hiyo kuelezea mafanikio na maboresho yaliyofanywa na chama cha ANC, ambacho kinakabiliwa na ushindani mkali katika uchaguzi ujao huku kikiwa katika hatari ya kupoteza kwa mara ya kwanza wingi wa wabunge.

    

"Tumefuatilia mageuzi ya ardhi, na kutoa mamilioni ya hekta za ardhi kwa wale waliopokonywa ardhi zao kwa nguvu, tumejenga nyumba, zahanati, hospitali, barabara na kujenga madaraja, mabwawa, na miundombinu kadhaa. Tumesambaza umeme na maji safi kwa mamilioni ya kaya za Afrika Kusini," alisema Ramaphosa.

Raia wa Afrika Kusini watapiga kura Mei 29, miongo mitatu baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994 uliotamatisha utawala kandamizi wa wazungu, na kumuweka madarakani Nelson Mandela na chama chake cha ANC.

Chama cha ANC mashakani

Kuanzia kushoto: Rais wa sasa wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, akifuatiwa na waliowahi kuliongoza pia taifa hilo Nelson Mandela na Jacob Zuma wote kutoka chama Cha ANC. Zuma kwa sasa ameanzisha chama chake kipya cha MK.Picha: Leon Neal/Getty Images; Getty Images; Phill Magakoe/AFP/Getty Images

Kura ya maoni iliyofanywa na shirika la Ipsos na iliyotolewa siku ya Ijumaa imeonyesha kuwa uungwaji mkono kwa chama tawala ANC, ambacho kilipata zaidi ya asilimia 57 ya kura katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019, umeshuka hadi zaidi ya asilimia 40.     

Iwapo ANC itapa ushindi ulio chini ya asilimia 50, basi chama hicho kitalazimika kutafuta washirika wa kuunda serikali ya mseto ili kusalia madarakani.

Taswira ya chama hicho imetiwa doa na shutuma za ufisadi na kushindwa kwake kukabiliana ipasavyo na umaskini, uhalifu,  ukosefu wa usawa  na ukosefu mkubwa wa ajira.

Ramaphosa alikiri matatizo hayo, lakini akawashutumu wakosoaji kwamba ni watu ambao wameamua "kufumba macho" kwa makusudi na hawayaoni mafanikio yao.     

"Tumepiga hatua kubwa na tumedhamiria kufanya mengi zaidi," alisisitiza rais huyo wa Afrika Kusini. 

Soma pia:  Miaka 15 tangu wazungu awalipoamua ku´ngoa utawala wa kibaguzi Afrika kusini

Takriban theluthi mbili ya waliohojiwa katika kura hiyo ya maoni ya Ipsos wamesema kuwa nchi hiyo ipo katika mwelekeo mbaya. 

Upinzani wajitutumua 

John Steenhuisen, mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Democratic Alliance (DA)Picha: MICHELE SPATARI/AFP

John Steenhuisen, mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), amesema katika hotuba yake katika jimbo la KwaZulu-Natal kwamba viongozi wa ANC "walitoa ahadi nyingi za matumaini, lakini walichofanikiwa kukileta ni jinamizi tu." 

Steenhuisen ameendelea kuwa uhuru wa kweli unawezekana pale tu unapokuwa na ajira inayoweza kukidhi mahitaji ya familia yako na kujenga mustakabali wa maisha bora.      

Ipsos imesema uungwaji mkono kwa chama cha DA ulikuwa karibu asilimia 22. Chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinatabiriwa kupata asilimia 11.5 ya kura, kikifuatiwa na chama kipya cha rais wa zamani Jacob Zuma cha Mkhonto we Sizwe (MK) ambacho kinatazamiwa kupata asilimia 8.4.

(Chanzo: AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW