1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yamjibu Trump kuhusu ardhi ya Afrika Kusini

John Juma AFPE, DPAE
23 Agosti 2018

Afrika Kusini imesema rais wa Marekani Donald Trump anapanda mbegu za mgawanyiko kufuatia ujumbe wake wa Twitter wa kutaka waziri wake kuchunguza hatua ya Afrika Kusini kuwapokonya watu ardhi na izigawe upya kwa watu.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa im Parlament
Picha: Getty Images/AFP/R. Bosch

Afrika Kusini imemshutumu rais wa Marekani Donald Trump kwa kupanda mbegu za migawanyiko, baada ya kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa wizara yake ya mambo ya nchi za nje itachunguza hatua ya unyang'anyi wa ardhi na mashamba pamoja na madai ya mauaji ya wakulima kwa kiwango kikubwa nchini Afrika Kusini.

Ujumbe wa Rais Donald Trump kwenye ukurasa wake wa Twitter, ulijiri baada ya taarifa iliyotangazwa katika kituo cha televisheni cha Fox News kuwa Afrika Kusini inapanga kubadilisha katiba yake. Ili kuharakisha hatua ya serikali kuchukua udhibiti wa ardhi na mashamba yanayomilikiwa na watu binafsi bila ya kuwafidia. Kama hatua ya kushughulikia suala la ukosefu wa usawa wa umiliki wa ardhi kwa msingi wa rangi.

Afrika Kusini: Mtazamo wa Trump ni finyu

Trump ataka hatua za serikali ya Afrika Kusini kuhusu ardhi ichunguzwePicha: picture-alliance/dpa/T. Everet

Trump aliongeza kuwa amemtaka waziri wa mambo ya nchi za nje Mike Pompeo kuchunguza kwa makini hali ilivyo.

Ujumbe wa Trump ambao uliambatanisha ukurasa wa Twitter wa mtangazaji habari wa Fox News Tucker Carlson ulisema "serikali ya Afrika Kusini sasa inatwaa ardhi ya wazungu ambao ni wakulima”

Saa chache baadaye, serikali ya Afrika Kusini ilijibu kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa "Afrika Kusini inapinga kikamilifu, huu mtazamo finyu, unaolenga tu kuligawa taifa letu, na kutukumbusha kuhusu enzi za nyuma za ukoloni”

Wakati uchaguzi mkuu wa mwaka 2019 ukikaribia, rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ameingilia kati kuharakisha mageuzi kuhusu umiliki wa ardhi, ili kuondoa dhuluma kuu za kihistoria dhidi ya Waafrika Kusini weusi ambao ndio wengi, kuanzia wakati wa ukoloni na utawala wa ubaguzi wa rangi uliomalizika 1994.

Wazungu wamiliki asilimia kubwa ya mashamba?

Wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi, raia weusi wa Afrika Kusini walizuia kumiliki ardhi katika sehemu nyingi nchini humoPicha: DW/T. Andrews

Miaka 24 baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, wazungu wa Afrika Kusini ambao ni asilimia nane ya idadi jumla ya nchi hiyo, wanamiliki asilimia 72 ya mashamba tofauti na asilimia nne pekee ya mashamba yaliyoko mikononi mwa watu weusi ambao ndio wengi zaidi nchini humo. Hayo ni kulingana na Rais Ramaphosa.

Ili kupata suluhisho la ukosefu huo wa usawa, rais alitangaza katika siku za hivi karibuni kuwa katiba itabadilishwa ili kuruhusu serikali kuchukua ardhi kisha igawiwe upya kwa watu lakini bila fidia kwa wamiliki wake wa sasa.

Mnamo mwezi Machi mwaka huu, waziri wa uhamiaji wa Australia Peter Dutton alizusha mzozo wa kidiplomasia na Afrika Kusini aliposema kuwa nchi yake inapaswa kuwapa kipau mbele wakulima wazungu wa Afrika Kusini wanaotafuta hifadhi kwa sababu wanapitia hali y akutisha

 

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW