1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yasitisha kuanza utoaji chanjo ya AstraZeneca

Sylvia Mwehozi
8 Februari 2021

Afrika Kusini imesitisha mipango ya kuanza utoaji chanjo ya AstraZeneca na Oxford baada ya utafiti kuonyesha kuwa chanjo hizo hazina ufanisi katika kuzuia magonjwa mepesi na ya wastani kutoka kwenye aina mpya ya virusi

Impfkampagne in Südafrika
Picha: Siphiwe Sibeko/AP Photo/picture alliance

Afrika Kusini ilipokea dozi milioni moja ya chanjo ya AstraZeneca wiki iliyopita na ilitarajiwa kuanza zoezi la kuwachanja wahudumu wa afya katikati ya mwezi huu. Matokeo ya awali na ya kukatisha tamaa yameashiria kuwa chanjo ya AstraZeneca inaweza isiwe na manufaa.

Matokeo ya utafiti huo mdogo uliofanywa na chuo kikuu cha Witwatersrand mjini Johannesburg, yanapendekeza kuwa chanjo ya AstraZeneca inatoa kinga kidogo dhidi ya "magonjwa mepesi na ya wastani" yanayosababishwa na aina mpya ya kirusi nchini Afrika Kusini. Waziri wa afya wa Afrika Kusini Zweli Mkhize amesema chanjo ya AstraZeneca inaonekana kuwa na ufanisi dhidi ya virusi vya mwanzo lakini sio hivi vinavyojibadili na hivyo wanasitisha zoezi hilo kwa muda.

Waziri wa afya wa Afrika Kusini Zweli MkhizePicha: Phill Magakoe/AFP/Getty Images

"Matokeo yanaonyesha kuwa kirusi kipya kilipunguza ufanisi kutoka maambukizi madogo hadi ya wastani, na hatujui athari ya chanjo kwenye magonjwa makali na kifo. Kazi zaidi inahitajika kufanywa juu ya ufanisi wa chanjo. Kwa sababu kuna matokeo kutoka nchi zingine ambayo yamekuwa ya kuridhisha kabisa lakini kuna maswala nchini Afrika Kusini ambayo tunahitaji kutafiti zaidi", alisema waziri wa afya.

Chanjo ya AstraZenecaPicha: Frank Augstein/AP Photo/picture alliance

Mkhize amesema wanasayansi wataendelea kufanya utafiti wa endapo chanjo ya AstraZeneca inaweza kuzuia ugomjwa mkali na vifo dhidi ya aina mypa ya kirusi. Maafisa wa afya wana wasiwasi na aina mpya ya kirusi cha Afrika Kusini ambacho kimekuwa na tabia ya kujibadili. Chanjo zingine zimeonyesha ufanisi mdogo dhidi ya aina hiyo mpya ya virusi ingawa zimetoa kinga nzuri ya magonjwa makali na kifo.

Wakati Afrika Kusini ikishikwa na wasiwasi kuhusu chanjo ya AstraZeneca, Australia imewahakikishia raia wake kuwa chanjo hiyo ina ufanisi katika lengo lake la awali. Waziri wa afya wa Australia Greg Hunt amesema "kwasasa hakuna ushahidi wowote unaonnyesha kupunguzwa kwa ufanisi wa chanjo ya AstraZeneca au Pfizer katika kuzuia magonjwa makali na kifo."

Australia inatarajia kuidhinisha matumizi ya chanjo hiyo ndani ya siku mbili zijazo. Mwezi uliopita iliidhinisha chanjo ya Pfizer -BioNTech. Kwingineko Ufaransa imeripoti kushuka kwa maambukizi mapya ya COVID-19 kwa siku ya nne mfululizo. Serikali ya Ufaransa imepinga wito wa kuanzisha tena awamu ya tatu ya vizuizi vya nchi nzima kutoka kwa watalamu wa afya wanaohofu kuwa aina mpya ya virusi inaweza kuzijaza hospitali.Ramaphosa: Afrika pia inahitaji chanjo ya COVID-19

Hapa Ujerumani mamia ya watu waliandamana Jumapili mjini Munich kupinga hatua za kupambana na virusi vya corona.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW