Katika muda wa siku tatu wageni walifurushwa na kuwapora
15 Aprili 2019Ripoti ya HRW ilieleza kwamba katika muda wa siku tatu Machi 25 hadi Machi 27 makundi ya watu waliokuwa na vyuma na marungu walivunja nyumba za raia wakigeni na kuwafurusha mjini Durban, Mashariki mwa Pwani ya Afrika kusini na kisha kupora mali zao.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, lilieleza kwamba kiasi cha watu sita waliuwawa na kadhaa kujeruhiwa hivyo kuzidisha hofu ya kuzuka tena kwa umwagaji damu wa raia wa kigeni katika taifa hilo ambalo masikini wasiokuwa na ajira wanawashutumu raia wakigeni kuchukua kazi zao.
Watu 88 raia wa Malawi walionusurika na mashambulizi hayo waliwaomba wawakilishi wa UNHCR kwamba wanataka kurudishwa nchini mwao Malawi huku wasiokuwa na budi wakirudi katika eneo hilo walilofukuzwa.
Mkurugenzi wa HRW nchini Afrika Kusini, Dewa Mavhiga alisema kuwarudisha wakimbizi katika jamii zao bila ya haki na uadilifu kufanyika kwa mashambulizi waliyofanyiwa ni kutengeneza janga.
Dewa alisema ili kuwakomesha wanaowashambulia raia wakigeni, kuna udharura wa kuwa na kanuni bora, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka akiongeza kwamba kutochukuliwa hatua kwa wahusika hao ni ukiukaji wa sheria katika uhalifu wa mashambulizi dhidi ya wageni.
HRW pia iliwataka wanasiasa kuepuka kutoa kauli za kuwasingizia wageni ambao waliingia katika nchi hiyo kinyuke cha sheria na kusema kauli hizo zinazochochea ghasia dhid ya wageni. Ripoti hiyo ililenga matamshi ya rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambapo katika mkutano wa hadhara wa chama chake mwezi Machi aliwalaumu wahamiaji ambao hawajasajiliwa kwa matatizo ya nchi hiyo na kusema watasakwa.
Ghasia dhidi ya wageni nchini humu zilipingwa kutoka kila pembe jambo lililopelekea kikao cha dharura baina ya waziri wa maswala ya kigeni Lindiwe Sisulu na waziri wa polisi Bheki Cele na wajumbe wengine kutoka mataifa ya Afrika.
Mamilioni ya raia wakigeni wanaishi Afrika Kusini, wengi kutoka Afrika na wengi hawajasajiliwa.
Wageni hao ndio wanapata makali ya hasira za raia weusi masikini wa Afrika Kusini wanaokumbwa na tatizo sugu la ukosefu wa ajira na kutokuwa sana kwa uchumi wao tangu kutamatika kwa uongozi wa raia wachache waupe mwaka 1994.
Hadi sasa kiasi cha raia wakigeni 62 wameuliwa tangu kuanza kwa wimbi la mashambulizi dhidi ya raia wakigeni mwaka 2008.
(AFPE)