Afrika Kusini yawaita nyumbani wanajeshi wake kutoka MONUSCO
16 Oktoba 2023Amri hiyo iliyotolewa siku ya Jumapili (Oktoba 15) imechukuliwa baada ya wanajeshi hao kutuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono na maonevu. Wanajeshi hao wataendelea kuwepo nchini Afrika Kusini hadi uchunguzi utakapomalizika.
Jeshi la Afrika Kusini limeongeza kuwa wachunguzi wamepelekwa nchini Kongo kufanya uchunguzi rasmi.
Soma zaidi: Walinda amani 8 wa UN wakamatwa Kongo kwa utovu wa nidhamu
Limesema inasikitisha kwamba serikali ya Afrika Kusini haikuarifiwa moja kwa moja kuhusu madai hayo lakini iliyafahamu kupitia kwenye vyombo vya habari.
Mapema wiki iliyopita, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema kuwa Kikosi cha Umoja huo nchini Kongo (MONUSCO) ulipokea ripoti kwamba wanajeshi wanaodaiwa kuhusika walikuwa wakikutana baada ya saa za marufuku ya kutoka nje, kwenye baa moja inayojulikana kuwa mahali ambapo ngono ya kibiashara inafanyika.