Afrika kuwa na msimamo wa pamoja Copenhagen.
12 Oktoba 2009Bara la Afrika litadai mabilioni ya dola kama fidia kutoka mataifa yanayochafua hewa na kusababisha ongezeko la ujoto barani humo. Kwa mujibu wa maafisa nchi za kiafrika madai hayo yatatolewa katika mkutano wa kilele wa umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa utakaofanyika mwezi Desemba mjini Copenhagen-Denmark.
Msimamo huo umechukuliwa katika mkutano maalum kwenye mji mkuu wa Burkina Faso-Ouagadougu, ambapo maafisa wa nchi za kiafrika wamekua wakikutana ,miezi miwili kabla ya mkutano huo wa umoja wa mataifa mjini Copenhagen.
Afrika kuwa na sauti moja:
Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Jean Ping aliuambia mkutano huo unaofahamika kama jukwaa la saba la dunia juu ya maendeleo endelevu, kwamba kwa mara ya kwanza Afrika itakua na msimamo wa pamoja.
Alisema " tumeamua kuzungumza kwa sauti moja na tutadai fidia kwa uharibifu wowote wa mazingira unaosababisha majanga ya kimaumbile barani mwetu." Kwa mujibu wa wataalamu eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni moja kati ya maeneo yalioathirika zaidi kutoka na ongezeko la ujoto duniani.
Bw Ping alisema nchi za Afrika zinatarajia mataifa ya viwanda yataahidi mkopo mpya wa kimataifa kuzisaidia nchi masikini, na akatoa mfano wa jimbo la Marekani la Texas ambalo likiwa na wakaazi milioni 30 linatoa gesi nyingi zinazoharibu mazingira, kuliko ukiwajumuisha waafrika bilioni moja kwa pamoja.
Rais Blase Campaore wa Burkina Faso alisisitiza kwamba bara la Afrika lina vikwazo vingi vya kukiuka, vinavyoambatana na ukosefu wa ufundi na utaratibu wa usimamiaji fedha na akatoa wito wa mkutano mkubwa wa nchi za kiafrika kuanzia 2010 na kuendelea kulijadili suala hilo.
Benki ya dunia inakadiria kwamba nchi zinazoendelea ziataathiria kwa asili mia 80 ya uharibifu ya mabadiliko ya hali ya hewa licha ya kuwa zinatoa karibu theluthi moja tu ya gesi zinazochafua mazingira.
Azimio la mwisho:
Katika azimio la mwisho viongozi wa mataifa sita waliohudhuria mkutano huo wamesema awameunga mkono wito wa kuyataka mataifa yaviwanda kupunguza utoaji gesi ya Carbon kwa kiasi ya asili mia 40 ifiakapo 2020 ikilinganishwa na viwango vya 1990.
Azimio hilo pia limetoa wito wa kulegezwa utaratibu na masharti kwa nchi za kiafrika,kuelekea suala la nafasi katika nyenzo za mfumo wa maendeleo ya kusafisha mazingira.
Chini ya utaratibu huo unaojulikana kwa kimombo kama Clean Development Mechanism-CDM, mataifa tajiri yalioidhinisha mkataba wa Kyoto yanaweza kupata mikopo kutoakana na miradi inayopunguza au inayozuwia utoaji wa gesi zinazochafua hali ya hewa katika nchi masikini.
Waziri wa mazingira wa Burkina Faso Salifou Sawadogo alisema bara la Afrika linahitaji dola 65 bilioni kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkutano huo wa Ouagadougou uliomalizika jana ulihudhuriwa na Marais wa Benin, Burkina Faso,Jamhuri ya Afrika kati, Congo, Mali na Togo.
Mwandsishi: M.Abdul-Rahman/afp
Mhariri:Sekione Kitojo