ECOWAS yawawekea vikwazo watawala wa kijeshi Guinea
17 Septemba 2021Wakuu hao wa mataifa wameamua kuzuwia mali za kifedha na kuwawekea marufuku ya kusafiri wanachama wa utawala wa kijeshi na ndugu zao, huku wakisisitiza juu ya kuachiliwa kwa rais Alpha Conde.
Rais wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, Jean Claude Brou alisema viongozi wakuu wa mataifa ya Afrika Magharibi wamesisitiza pia kwamba hakupaswi kuwepo na haja ya kipindi kirefu cha mpito kwa taifa hilo kurejea kwenye mkondo wa kidemokrasia.
"Kipindi cha mpito laazima kiwe kifupi, na wamesisitiza hata kwamba hakipaswi kudumu zaidi ya miezi sita, hivyo katika miezi sita, uchaguzi unapaswa kufanyika.
Soma pia: Watawala wapya Guinea watafuta kujiimarisha madarakani
Wanasisitiza hilo kwa sababu uchuguzi utaruhusu kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba katika jamhuri ya Guinea," alisema Brou katika taarifa.
Shinikizo la kuachiwa Alpha Conde
Vikwazo hivyo vinavyolenga watu makhsusi vinakuja baada ya viongozi wa mapinduzi kutaja masharti kadhaa ya kumuachia Conde, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Ghana.
Tayari ECOWAS ilikuwa imeonya kwamba ingewaadhibu watawala wa kijeshi endapo hawangemuachia Conde, ambaye anazuwiliwa katika eneo lisilojulikana tangu alipokamatwa wakati wa mapinduzi ya Septemba 5 mjini Conakry.
Soma pia: Umoja wa Afrika waisimamisha uanachama Guinea kwa muda
ECOWAS imetoa wito pia kwa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuunga mkono vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi, unaojulikana kama Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Maendeleo au kwa kifupisho chake cha Kifaransa CNRD.
ECOWAS ilikuwa imetuma ujumbe nchini Guinea wiki iliyopita kukutana na kiongozi wa mapinduzi Luteni Kanali Mamady Doumbouya, na ilikuwa inasubiri kuchukuwa uamuzi juu ya namna ya kuushinikiza utawala wa kijeshi kurudi kurudi kwenye utawala wa kikatiba.
Mashauriano ya kitaifa Guinea
Siku ya Jumanne, utawala wa kijeshi ulianzisha mazungumzo ya siku nne pamoja na makundi mbalimbali kujadili njia ya kurudi kwenye utawala wa kiraia.
Luteni-Kanali Doumbouya na maafisa wake wamekutana mpaka sasa na viongozi wa kisiasa, mamlaka za kidini na wanaharakati wa haki za binadamu, na walitarajiwa kuzungumza na wanadiplomasia wa kigeni, vyama vya wafanyakazi na watendaji wa sekta ya madini siku ya Ijumaa.
Soma pia: Jeshi la Guinea laanza kujadili mustakabali wa taifa hilo
Wakuu wa mataifa pia wameongeza mbinyo dhidi ya serikali ya mpito ya Mali, wakiitaka kuheshimu makubaliano ya kuandaa uchaguzi wa Februari 2022, na kuwasilisha mpango wa uchaguzi kufikia mwezi ujao, kwa mujibu taarifa ya baada ya mkutano wa kilele wa jana.
Chanzo: Mashirika