Afrika Mashariki yafanya vyema kibiashara - Benki ya Dunia
25 Oktoba 2016Kulingana na ripoti ya benki ya dunia iliyotolewa alasiri ya leo, Rwanda, Uganda, Tanzania na Kenya zimetekeleza mikakati ambayo imechangia pakubwa katika kuwapunguzia dhiki wafanyabiashara kuendesha shughuli zao.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa, ni kurahisisha upatikanaji wa vibali vya kuanzisha biashara, kuharakisha michakato ya kutoza kodi kwenye mamlaka za forodha na mipakani, pamoja na kuondoa baadhi ya masharti.
Katika ripoti yake, Benki ya Dunia inasema hatua hizi zimesababisha bidhaa kusafirishwa kwa siku chache kuliko hapo awali kutoka bandari kama ile zile za Mombasa, Kenya, na Dar ss Salaam, Tanzania, hadi mataifa ya barani ya Rwanda, Uganda, Burundi na kwingineko.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rwanda iko katika nafasi 56 kati ya mataifa 190 duniani huku ikiongoza barani Afrika, Kenya inashikilia nafasi ya 92, Uganda iko katika nafasi ya 115 ikilinganishwa na 122 mwaka uliopita.
Ingawa Tanzania iko katika nafasi ya 132, inasifiwa kuwa na mazingira bora ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara.