Afrika na Gaddafi: "Hatuwezi kuwa wizi wa fadhila"
25 Machi 2011Kwa miongo kadhaa sasa, kiongozi huyo amekuwa akiwekeza katika miradi mikubwa mikubwa ya ujenzi wa miundombinu, huduma na usafiri katika bara hilo. Kampuni ya taifa ya mafuta ya Libya, peke yake, ina mtandao wa matangi 2000 ya mafuta katika nchi 20 za Afrika.
Ni rahisi kwenye nchi za Afrika kukuta barabara inaitwa mtaa wa Gaddafi, au msikiti wa Gaddafi, au jengo la Gaddafi, maana nchi nyingi za bara hilo zinamtukuza kiongozi huyu.
Na hili, hapana shaka, linaonesha namna ambavyo Gaddafi amekuwa na ushawishi katika sehemu kadhaa za bara hilo.
Kwenye Benki ya Maendeleo ya Afrika, Libya peke yake ina mtaji wa euro milioni 260, jambo ambalo mwakilishi wa benki hiyo kwa kanda ya Afrika ya Kaskazini, Emanuele Santi, anaona kuwa halitabadilika.
"Libya ni mshirika muhimu kwenye benki yetu. Sifikirii kuwa Gaddasi atazitoa fedha zake, maana daima amekuwa akionesha mshikamano na bara la Afrika na kwa hivyo hawezi kubadilika. Na sisi pia hatukusudii kuzizuia fedha zake."
Kwa ujumla, thamani ya vitega uchumi mbalimbali vya Libya kwenye nchi mbalimbali za Afrika inafikia euro bilioni sita. Miradi na makampuni kadhaa makubwa yanafaidika na mkopo wa kifedha kutoka Libya.
Mfano ni kampuni ya simu za mkononi ya Uganda Telecom, ambayo mbili ya tatu ya hisa zake inamilikiwa na Mamlaka ya Uwekezaji ya Libya, ambayo thamani yake ni karibuni euro milioni 10.
Na kama hilo halitoshi, katika miaka ya hivi karibuni, Gaddafi, ambaye mwenyewe aliwahi kujiita mfalme wa wafalme, aliahidi mabilioni zaidi ya euro kuwekezwa kwenye uchumi wa bara la Afrika.
Miongoni mwa wanufaikaji wakubwa wa uwekezaji huu ni nchi ya Burkina Faso iliyoko magharibi mwa Afrika. Hapa Gaddafi amejenga miundombinu na hospitali kubwa kabisa.
Tangu zamani, serikali ya nchi hii imekuwa na mahusiano makubwa sana Gaddafi, jambo ambalo hata kiongozi wa Muungano wa Upinzani, Hama Arba Diallo, hana sauti ya kupingana nalo sana.
“Kuna uwekezaji mkubwa kama ule wa chuo kikuu, ambao serikali yetu peke yake isingeliweza kuumudu, lakini Muammar Gaddafi ametusaidia. Na hajawekeza hapa Burkina Faso tu, bali pia kwenye nchi nyengine nyingi za Afrika, na kwa hilo tunamshukuru sana. Kinachotokea Libya hivi sasa, kinatusikitisha sote. Lakini hakuna nchi ya Afrika ambayo Gaddafi ameisaidia kifedha, ambayo leo itakuwa mwizi wa fadhila kwake."
Kwa umoja na utegemezi huu wa kiuchumi uliopo, si jambo la ajabu kwamba nchi za Kiafrika hazinyanyui sauti sana kupinga yale yanayofanywa na Gaddafi dhidi ya raia wake.
Wataalamu wa mambo ya siasa za Afrika, wanaona kuwa isitegemewe kwa siku za karibuni, viongozi wa Afrika watamuwacha mkono Gaddafi.
"Gaddafi amejijenga sana Afrika, kupitia anavyozungumzia uzalendo wa Kiafrika, kupitia ujenzi wa misikiti Afrika nzima. Na kusema kwamba hili linaweza kubadilika kwa haraka, bado ni suala la kuangaliwa." Anasema Helmut Asche, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mambo ya Afrika ya mjini Leipzig.
Mwandishi: Salamata Sänger/ZR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo