Afrika yajizatiti kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia
26 Novemba 2007Malengo hayo manane yaliidhinishwa na viongozi mbalimbali duniani kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mnamo mwaka wa 2000. Malengo hayo yanatazamiwa kufikiwa ifikapo mwaka wa 2015. Kandoni mwa mkutano wa jumuiya ya madola, Commonwealth, naibu katibu mkuu wa kampeni ya milenia barani Afrika, Tajudeen Abdul- Raheem, alizunguzia juu ya uwezekano ya bara la Afrika kuyafikia malengo hayo.
Malengo ya maendeleo ya milenia yanalenga kupunguza kwa asilimia hamsini njaa na umaskini, kuhakisha watoto wanapata elimu ya shule ya msingi, kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake. Vile vile yanalenga kupunguza idadi ya vifo vya watoto na akina mama wakati wa uzazi, kupambana na ukimwi, malaria na magonjwa mengine, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuunda ushirikiano wa kimaendeleo wa kimataifa utakaozingatia maswala muhimu yakiwemo vikwazo vya kibiashara na madeni ya nchi.
Kama ripoti ya mwaka huu kuhusu malengo ya milenia inavyoonyesha, ufanisi katika kuyafikia malengo ya milenia kwa ujumla umepatikana. Hata hivyo kundi moja tu miongoni mwa makundi manane yaliyotajwa katika ripoti hiyo liko katika njia sawa katika kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia. Upungufu umedhihirika zaidi barani Afrika.
Kampeni ya milenia ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa mnamo mwaka wa 2002 kuwasaidia wananchi wazishawishi serikali zao ziyafikie malengo ya milenia. Naibu mkurugenzi wa kampeni hiyo barani Afrika, Tajudeen Abdul- Raheem, kandoni mwa mkutano wa jumuiya ya madola, Commonwelath, uliomalizika Jumapili iliyopita mjini Kampala Uganda alizungumza na shirika la habari la IPS kuhusu uwezo wa bara la Afrika kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia.
Alipoulizwa ni wapi kulipokuwa na ufanisi barani Afrika kuhusiana na malengo ya milenia, Abdul- Raheem amesema kwa kuangalia nchi moja moja kumekuwepo ufanisi hasa katika elimu, vifo vya watoto na ukimwi. Nchi kama Uganda inatoa elimu ya bure katika shule ya msingi na ya upili. Mamilioni ya watoto ambao hawakuweza kwenda shule sasa wanasoma. Malawi, Kenya, Nigeria, Afrika Kusini na Ghana zimepiga hatua kubwa pia katika kutoa elimu ya shule ya msingi, ingawa bado kuna changamoto nyingi.
Nchi kama vile Malawi ambayo ilikuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, imepunguza idadi ya watoto wanaokufa wakati wa kuzaliwa kwa asilimia 30, hivyo kuchukua nafasi ya pili duniani baada ya Peru. Rwanda inaendelea vizuri katika kuyafikia malengo ya milenia, ikiwa ni pamoja na elimu, teknolojia na kuwawezesha wanawake. Ina idadi kubwa ya wanawake bungeni kuliko nchi nyingi za magharibi. Hii inaonyesha ikiwa maswala haya yatapewa kipaumbele na kuwpo ari ya kisiasa, inawezekana kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia.
Tajudeen Abdul-Raheem amesema moja kati ya kashfa kubwa katika utekelezaji wa malengo ya milenia na ambalo makundi ya kijamii na vyombo vya habari vinatakiwa kuishughulikia, ni malengo ya milenia yanayohusiana na wanawake. Ama kweli malengo yote ya milenia yanawahusu wanawake kwa kuwa ndio wengi, na kwa hiyo maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana iwapo wanawake hawatahusishwa kikamilifu na kuwezeshwa.
Abdul- Raheem amesema kwa kutoa chanjo kwa wakati muafaka, vyandarua vya kuzuia mbu na kufanya juhudi nyengine, nchi nyingi kama vile Malawi zimefaulu kupunguza idadi ya vifo vya watoto. Lakini katika nchi nyingi baani Afrika, kasi ya wanawake wanaokufa wakati wa uzazi ni kubwa mno, hivyo kuzusha swali, ikiwa watoto wanaishi kwa muda mrefu kwa nini akina mama wanakufa?
Malengo ya milenia si jukwaa la kulishughulikia tatizo hili. Wanawake wengi hufariki kutokana na matatizo wakati wa kujifungua. Wengi zaidi hufariki kutokana na ukosefu wa usafiri kwenda katika vituo vya afya. Ikiwa utalazimika kumsafirisha mama mjamzito kutumia baiskeli, wakati atakapofika kwenye kituo cha afya, atakuwa mekufa.
Nchi tajiri duniani zimesaidia kuyafikia malengo ya milenia kwa kuyafuta madeni ya baadhi ya nchi kama vile Malawi, Uganda na Ghana. Fedha ambazo zilikuwa zitumike kulipa madeni zimeelekezwa kugharimia miradi ya kijamii na kiuchumi. Lakini Abdul- Raheem amesema kitisho kikubwa cha nchi tajiri ni ukosefu wa usawa wa kibiashara katika ngazi ya kimataifa, huku bara la Afrika likipata hasara kubwa kutokana na vikwazo vingi vya kibiashara.