Afrika yalalamikia ubaguzi dhidi ya weusi China
11 Aprili 2020Baadhi ya Waafrika katika kitovu hicho cha kibiashara wameripoti kuondolewa kwa nguvu majumbani mwao au kugabuliwa kutokana na hofu ya virusi vya corona. Na tadhahari ya usalama iliyotolewa na ubalozi wa Marekani leo imesema kuwa "polisi wameamuru mabaa na mikahawa kutowahudumia wateja wanaoonekana kuwa wa asili ya Kiafrika," na maafisa wa eneo hilo wameanzisha shughuli ya upimaji wa lazima na kumuweka katika karantini yeyote mwenye mahusiano na Waafrika.
Kuongezeka kwa visa vya virusi hivyo nchini China kumehusishwa kwa kiasi kikubwa na watu wanaowasili kutokea ng'ambo.
Wanadiplomasia wa nchi za Afrika mjini Beijing wamekutana na wizara ya mambo ya kigeni ya China na "kueleza wasiwasi wao na kulaani vikali matukio ya kusikitisha na kudhalilisha wanayopitia raia wetu,” Imesema taarifa ya ubalozi wa Sierra Leone mjini Beijing Ijumaa, na kuongeza kuwa raia 14 wamewekwa katika karantini ya lazima ya siku 14.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Nigeria Geoffrey Onyeama amesema amemuita balozi wa kuelezea wasiwasi mkubwa na kutaka serikali kuchukua hatua ya haraka.
Ghana imemuita balozi wa China wakati Waziri wa Mambo ya Kigeni Ayirkor Botchwey akilaani matendo hayo yasiyo ya kiutu.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema amemuita balozi wa China katika AU, Liu Yuxi kuelezewa "wasiwasi wao mkubwa.”
Kenya pia imezungumzia suala hilo. Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni imetaja "matukio yasio ya haki dhidi ya wageni, hasa wa asili ya Kiafrika,” kutoka kwa baadhi ya wenyeji wa Guangzhou, hasa wamiliki wa nyumba za kukodi.
Taarifa hiyo imesema ubalozi wa China mjini Nairobi umeiambia wizara ya mambo ya kigeni ya Kenya kuwa maafisa mjini Guangzhou wamepewa jukumu la kuchukua hatua ya haraka kuzilinda haki halali za Waafrika wanaohusika.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni ya China Zhao Lijian aliwaambia wanahabari Alhamisi kuwa jukumu la dharura la China ni kuzuia maambukuzi ya virusi hivyo yanayoingizwa na wageni lakini akakiri kuwa huenda kukawa na kutoelewana katika utekelezaji wa hatua zinazochukuliwa. Alisema China inawachukulia sawa wageni wote.