Afrika yapinga kukosekana usawa katika upatikanaji wa chanjo
10 Desemba 2020Onyo la afisa huyo linatolewa bara la Afrika lenye wakaazi bilioni 1.3 likikabiliwa na wimbi la pili la maambukizi ya COVID-19, na nchi kama Uingereza zikiwa tayari zimeanza kutoa chanjo dhidi ya maradhi hayo.
Nkengasong ameonya kuwa Afrika inaweza isifikiwe na chanjo hiyo hadi angalau baada ya mwezi Juni mwaka ujao wa 2021.
Soma zaidi: Uingereza yakamilisha maandalizi utoaji chanjo ya COVID-19
Ameutaka Umoja wa Mataifa kuitisha kikao maalum cha kujadili uadilifu katika kutengeneza na kusambaza chanjo ya COVID-19, ili kuepusha mgawanyiko unaodhihirika katika usambazaji wa bidhaa za kawaida baina ya nchi tajiri na maskini, lihusikapo suala la chanjo.
Bega kwa bega katika vita dhidi ya corona
''Ushindi dhidi ya COVID-19 hautapatikana katika nchi za magharibi pekee'' ametahadharisha Nkengasong na kukosoa ''mjadala wenye mashaka'' unaoendelea wakati nchi tajiri zikijilimbikizia dozi za chanjo zinazopindukia mahitaji yao, wakati huo huo Afrika ikihangaika na mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kwamba angalau sehemu ya chanjo iliyopo inaweza kuzifikia hata nchi zinazoendelea. Mpango huo unajulikana kama COVAX.
Soma zaidi: Msalaba Mwekundu laonya kuhusu habari za uongo za chanjo ya COVID-19
Kulingana na mkuu huyo wa Africa CDC, kupitia mpango huo Afrika haitarajii kupata dozi za chanjo za kutosha kuwapa kinga asilimia 60 ya watu wake, kiwango kinachotakikana kuweza kusimamisha kusambaa kwa janga la COVID-19.
Ametumia fursa hiyo kuzitaka nchi zitakazopata dozi za chanjo ambazo ni zaidi ya mahitaji yao kuitoa ziada hiyo kwa nchi maskini kupitia mpango wa COVAX, kwa sababu ikiwa itachukua muda mrefu kabla ya chanjo hiyo kufika barani Afrika, virusi vya corona vinaweza baadaye kuwa tatizo sugu.
Wimbi la pili la maambukizi labisha hodi Afrika
Katika tangazo jingine linalohusiana na kauli hiyo ya John Nkengasong, Richard Mihigo ambaye ni afisa katika shirika la afya ulimwenguni, WHO, amesema litakuwa tatizo kubwa ikiwa baadhi ya nchi zitashikilia viwango vya ziada za chanjo na kuziacha nyingine mikono mitupu.
Soma zaidi:Merkel ana wasiwasi na utolewaji sawa wa chanjo ya COVID-19
Nchi 54 za bara la Afrika zimerekodi jumla ya maambukizi milioni 2.3 ya COVID-19, vikiwemo visa vipya 100,000 vilivyothibitishwa mnamo wiki moja iliyopita.
''Ni dhahiri kwamba Afrika inakabiliwa na wimbi la pili la maambukizi ya COVID-19, hakuna shaka juu ya hilo,'' amebainisha John Nkengasong, na kuongoza kuwa Afrika inapita katika kipindi kigumu kabisa katika historia yake.
Alipokuwa akiyasema hayo, mkutano wa shirika la biashara duniani, WTO ulikuwa ukifanyika mjini Geneva, kulijadili pendekezo la Afrika Kusini na India la kutaka kibali cha kukiuka kwa muda sheria za haki miliki, kuwezesha utengenezaji na usambazaji wa chanjo ya COVID-19 utakaowanufaisha mamilioni ya watu katika nchini zinazoendelea.
ape, afpe