1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yajinasua kutoka mitazamo ya kikoloni

21 Septemba 2026

Azimio la UN la kutumia ramani zinazoonyesha ukubwa halisi wa Afrika, mabadiliko ya mitaala na kampeni za kuonyesha mafanikio vinaanza kubadili namna bara hilo linavyoonekana duniani.

DW 2026 | Afrimaxx | Mabadiliko kupitia ubunifu: Jumba la sanaa nchini Nigeria
Wasanii ni miongoni mwa Waafrika wanaoishi barani na katika ughaibuni wanaosaidia kuonyesha taswira pana na yenye uhalisia zaidi kuhusu Afrika.Picha: DW

Azimio la Correct the Map, lililoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mjini New York mwanzoni mwa Septemba, limekuwa mafanikio makubwa kwa mataifa ya Afrika yaliyoendesha kampeni hiyo.

Nchi 164 wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ziliunga mkono matumizi ya ramani zinazoonyesha ukubwa halisi wa mabara, kama ramani ya Equal Earth, badala ya ramani ya Mercator iliyobuniwa katika karne ya 16.

Ramani ya Mercator imekuwa ikikosolewa kwa kupotosha ukubwa wa maeneo mbalimbali duniani. Huyaonyesha mataifa yaliyo karibu na ncha za dunia kuwa makubwa zaidi, huku Afrika na maeneo mengine yaliyo karibu na ikweta yakionekana madogo kuliko ukubwa wake halisi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo Robert Dussey, ambaye nchi yake iliwasilisha kampeni ya Correct the Map katika Umoja wa Mataifa, alisema uamuzi huo umeleta "hisia ya fahari.” Kampeni hiyo pia inaungwa mkono na Umoja wa Afrika.

"Hatimaye Afrika inapigania kurejesha nafasi yake katika jumuiya ya mataifa,” Dussey aliiambia DW. "Nafasi ambayo Afrika imepewa hadi sasa si ya haki. Haiakisi hali halisi ya bara hilo kihistoria, kijiografia wala kiuchumi.”

Kuondoa ukoloni katika uzalishaji wa maarifa

Kwa Dussey, mjadala kuhusu ramani za dunia hauishii katika jiografia. Unahusu pia namna maarifa, utamaduni na utambulisho vinavyojengwa, pamoja na mitazamo kuhusu nguvu za kisiasa na kiuchumi.

Marekani ndiyo nchi pekee iliyopiga kura dhidi ya azimio hilo. Rais Donald Trump pia ametumia majina ya maeneo kama sehemu ya siasa za alama. Ametoa maagizo ya kubadili jina la Ghuba ya Mexico na kuiita Ghuba ya Amerika, pamoja na Ziwa Ontario kuitwa Ziwa Amerika.

Mwanahistoria wa Ufaransa Romain Tiquet, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Dunia za Afrika, IMAF, anasema azimio hilo ni sehemu ya mjadala mpana wa kimataifa kuhusu kuondoa athari za ukoloni katika maarifa.

"Tangu mwishoni mwa miaka ya 2000 na mwanzoni mwa miaka ya 2010, kumekuwa na mijadala mingi kuhusu kuondoa ukoloni katika maarifa—vyuoni, katika makumbusho, taasisi za utamaduni, harakati za kijamii na asasi za kiraia,” alisema.

Kwa mujibu wa Tiquet, mijadala hiyo inahoji ni nani aliyeunda mifumo inayotumiwa kuutazama ulimwengu, aliitengeneza akiwa wapi na mifumo hiyo imesababisha mahusiano gani ya nguvu. Suala la ramani linaingia moja kwa moja katika mjadala huo.

Ramani ya Equal Earth inalenga kuuonyesha ulimwengu kwa uwiano sahihi zaidi wa ukubwa wa mabara na maeneo mbalimbali.Picha: Equal Earth/Handout/AFP

Mali yajitenga na ushawishi wa Ufaransa

Mataifa mengi ya Afrika pia yanajaribu kuondoa athari za ukoloni katika mifumo yao ya elimu. Wakati mwingine hatua hizo zinachochewa na mabadiliko ya kisiasa.

Oktoba 2025, serikali ya Mali iliamua kuondoa historia ya Ufaransa katika mitaala ya shule. Mapinduzi ya Ufaransa hayatafundishwa tena, huku mkazo ukiwekwa katika historia ya Mali na falme za kale za Afrika Magharibi.

Katika kipindi cha miaka michache, serikali ya kijeshi ya Mali imejitenga kwa kiasi kikubwa na Ufaransa, iliyokuwa mkoloni wake. Mwaka 2022, Mali ilisitisha ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa na wanajeshi wa Ufaransa wakaanza kuondoka nchini humo.

Burkina Faso na Niger pia zilichukua hatua kama hizo. Mwaka 2023, nchi hizo tatu ziliunda Muungano wa Mataifa ya Sahel, AES.

Mwanahistoria Philemon Mtoi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira nchini Tanzania anasema Mali imechukua hatua muhimu.

"Ninaamini kwamba nchi isiyo na uelewa mkubwa wa historia yake ni sawa na nchi isiyo na uongozi au mwelekeo ulio wazi,” alisema. "Uamuzi huu ni muhimu kwa sababu unalenga kuimarisha uzalendo na kujenga utambulisho imara zaidi wa kitaifa.”

Je, Ulaya inapaswa kulipa kwa utumwa wa Atlantiki?

02:01

This browser does not support the video element.

Historia ya Afrika kutoka mtazamo wa Waafrika

Mtoi anasema kwa kuwekeza katika utafiti na uhifadhi wa historia ya Afrika, Mali—kama ilivyo Afrika kwa ujumla—inaimarisha mchango wake katika uzalishaji wa maarifa duniani.

Kwa muda mrefu, historia ya Afrika imeandikwa kupitia mitazamo ya wavamizi na watawala wa kikoloni. Mtoi anasema kuirejesha na kuiandika historia hiyo kutoka katika mtazamo wa Waafrika si tu hatua ya kuondoa urithi wa ukoloni, bali pia ni njia ya kuelekea uhuru wa kifikra na kujiamini kiutamaduni.

Kwa mujibu wake, nchi nyingine nyingi za Afrika, zikiwemo Ghana, Namibia, Afrika Kusini na Kenya, zimeanza kufuata mwelekeo kama huo.

Tanzania pia imefanya mabadiliko makubwa katika mitaala yake ya shule. Somo la lazima la Historia ya Tanzania na Maadili limechukua nafasi ya historia ya dunia na litafundishwa kwa Kiswahili, lugha ya taifa.

Hata hivyo, Mtoi anaonya kuwa maarifa kuhusu mataifa mengine na historia ya dunia hayapaswi kufutwa kabisa. Anasema ni muhimu pia kufahamu matukio makubwa kama Mapinduzi ya Ufaransa, ingawa yanaweza kufundishwa kwa kina katika hatua za juu za elimu.

UN kutambua biashara ya utumwa kuna tija kwa Afrika?

04:35

This browser does not support the video element.

Gharama ya mitazamo potofu kuhusu Afrika

Elimu rasmi ni sehemu moja tu ya juhudi hizo. Shirika lisilo la faida la Africa No Filter, ambalo lilishiriki kuanzisha kampeni ya Correct the Map, linafanya kazi ya kupinga na kubadili simulizi potofu kuhusu Afrika.

Katika ripoti yake yenye kichwa "Gharama ya mitazamo ya vyombo vya habari kwa Afrika,” shirika hilo linasema bara la Afrika linaweza kuwa linapoteza hadi dola bilioni 4.2 kila mwaka kupitia malipo makubwa ya riba kutokana na habari zenye upendeleo.

François Bouda, afisa wa sanaa na utamaduni katika Africa No Filter, anasema vyombo vya habari vinaendelea kuionyesha Afrika kama bara la umaskini, ufisadi na migogoro.

Wanawake 5 wa Kiafrika wanaobadilisha dunia

03:20

This browser does not support the video element.

Shirika hilo limeanzisha kampeni ya #NotWaiting ili kubadili mtazamo huo ndani na nje ya Afrika.

"Tunawalenga kwanza Waafrika kwa sababu sisi pia tunapaswa kubadili namna tunavyolitazama bara letu,” alisema Bouda. "Tumekubali taswira ya bara lisiloweza kujihudumia, ambalo ni maskini na halina fursa. Tumeingiza mtazamo huo ndani yetu na kuanza kuuamini, ingawa mambo mengi mazuri yanaendelea kutokea.”

Afrika haisubiri wengine waionyeshe njia

Kampeni ya #NotWaiting ni sehemu ya harakati pana zinazolenga kuonyesha maendeleo, mipango ya kisiasa, ubunifu na watu wanaochangia mabadiliko barani Afrika.

Kampeni hiyo inawaangazia Waafrika walioko barani na katika ughaibuni ambao, kwa mujibu wa Bouda, "hawasubiri nguvu kutoka nje iwaelekeze njia ya kufuata.”

Anasema watu wengi tayari wanafanya mambo makubwa kwa manufaa ya Afrika, lakini tatizo ni kwamba hawaonekani.

Nduna Mkomanile, shujaa wa kike Tanzania enzi ya ukoloni

01:48

This browser does not support the video element.

Kupitia kampeni hiyo, Waafrika wenyewe wanachora taswira chanya ya bara linalobadilika. Kila mtu anaweza kushiriki simulizi yake bila kutegemea taasisi za kimataifa au vyombo vya habari kuamua habari inayopaswa kusimuliwa.

"Tumeendelea kujenga wakati wote,” unasema ujumbe wa video ya kampeni hiyo. "Kuanzia barabara za vijijini hadi miji yenye msongamano, katika nchi 54 za bara hili, mamilioni ya watu wa kawaida wanafanya mambo ya kipekee kila siku.”

Kwa Africa No Filter na wanahistoria kama Philemon Mtoi, kubadili mtazamo kuhusu Afrika hakutabadilisha fikra pekee. Kunaweza pia kuleta mabadiliko halisi ya kiuchumi na kisiasa—na hatimaye kuipa Afrika nafasi inayostahili duniani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW