Afueni kwa Uhispania
11 Juni 2012Hata hivyo, aina hii ya manusura inaficha miripuko ya aina fulani kwa nchi zinazotumia sarafu ya Euro.
Jee mtu anahitaji kuifahamu dunia? Tazama: serikali ya Uhispania inatangaza kufilisika kwa sehemu, inataja kwamba peke yake haiwezi kuinusuru sekta ya mabenki katika nchi hiyo. Kutokana na kukiri huko, serikali hiyo inamiminiwa sifa kutoka duniani kote. Bei za hisa za mabenki zinapanda. Pia sarafu ya Euro inapata uimara. Michael Hüther, mkurugenzi wa taasisi ya Uchumi wa Ujerumani, anaweka wazi kwamba kutokana na hatua hiyo, Ulaya imedhihirisha kwamba inaweza kuchukua hatua kwa pamoja. Kwa mujibu wa Michael Hüther ni kwamba Uhispania kwa muda sasa imekuwa ikitegemea masoko ya fedha kupata mikopo na imebidi ilipe riba za juu kutokana na madeni yaliotokana na ule ukweli kwamba wawekezaji hawajataka kuona serikali ya Uhispania inafilisika.
" ... hiyo inatokana pia na hatari ya uhai wa sarafu ya Euro. Wanunuzi wa hisa waziwazi walikuwa hawako tayari kununua hisa za makampuni ya Uhispania, wakidhani kwamba mwishowe hawatalipwa fedha zao kwa sarafu ya Euro."
Wasiwasi huo kwa sasa umepungua miongoni mwa wawekezaji. Lakini athari ya dawa hii ya sasa ya kutuliza mambo inaweza ikapotea hewani kwa haraka. Msikilize mwanauchumi mkuu Benki ya Commerz hapa Ujerumani, Jörg Krämer, anavosema:
" Sisi pia hapo zamani tumeona vipi Ireland na Ureno zilivokwenda chini ya mwavuli wa kuokoa uchumi wa nchi hizo. Kwanza kabisa kuna afuweni, kwa vile ile hatari ya kuziambukiza nchi nyingine inazuliwa, na hali hiyo inaendelea hivyo kwa masiku kadhaa. Lakini siamini kwamba hali hiyo ni ya kudumu. Kwa hivyo tatizo la Uhispania halijaondoka."
Mabenki ya Uhispania yanakalia mlima wa madeni yasioweza kulipwa ambayo yamesababishwa na kuporomoka sekta ya biashara ya majumba katika nchi hiyo, na hali hiyo inazidi kuwa mbaya. Serikali ilipambana na nakisi katika bajeti, na haijaweza kudhibiti tena shughuli za mabenki ya nchi hiyo. Katika kila Wahispania wanne, mmoja hana ajira, pia uchumi unasambaratika. Mwezi April uzalishaji viwandani, ukilinganisha na mwaka uliopita, ulikwenda chini kwa asilimia nane. Kwa mujibu wa Jörg Krämer ni kwamba siasa za kukaza mkaja sio sababu ya kwenda chini uchumi:
" Kinyume chake. Uhispania haijapunguza matumizi katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu kwa vile kulikuweko na chaguzi katika mikoa ya nchi hiyo. Na hiyo ndio sababu kubwa kwanini Uhispania iko nyuma katika ile ahadi iliotolewa ya kupunguza nakisi ya bajeti ya serikali. Hiyo tena ndio sababu ya tatizo la kiuchumi na la kuaminika katika masoko."
Na japokuwa serikali ya Uhispania hadi sasa imezorotesha mambo katika siasa zake za uchumi na fedha, hata hivyo haijalazimika kuhofia kupewa masharti magumu kupata fedha hizo za kuyaokoa mabenki yake. Hiyo ni hali mpya katika zoezi hili la kuokoa uchumi wa nchi zilizoelemewa katika eneo la sarafu ya Euro. Wakati mabingwa wa kutoka Tume ya Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, wamekuwa wakiwachunguza wapangaji bajeti wa Ugiriki, Ireland na Ureno wanafanya nini na pia kuweza hata kujiingiza na kutoa usemi kuhusu siasa za kiuchumi za nchi hizo, huko Uhispania mabingwa hao wanaweza tu kudhibiti mambo na kujiingiza kuhakikisha kama marekebisho katika sekta ya taasisi za fedha yanafanyika ama sivyo. Kwamba uchumi wa Uhispania, ambao ni wanne kwa ukubwa katika Ulaya, umepata masharti hayo nafuu yadhihirisha safari hii ya muungano wa sarafu ya Ulaya inakoendea. Kwa mujibu wa mwanauchumi Jörg Krämer ni kwamba yaonesha hatua kwa hatua eneo la Euro linageuka kuwa eneo la Muungano wa kusafirisha fedha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na pia kuwa muungano wa kuweka dhamana pale mmoja wa wanachama anapokaribia kufilisika. Mwanauchumi huyo anahoji kwamba madeni kuyafanya ni ya wanachama wote wa muungano wa sarafu ya Euro haina maana kwamba nchi hizo zenye madeni zitarejea kuona uchumi wao ukikua.
Mwandishi: Zhang Danhong/ Othman, Miraji/ZR
Mhariri. Saumu Yusuf