1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Agizo la Trump lawaathiri mamia ya wasafiri

Caro Robi
29 Januari 2017

Agizo la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha mpango wa wakimbizi na kuwazuia wasafiri kutoka mataifa saba ya Kiislamu kuingia Marekani yamesababisha ghadhabu na hali ya sintofahamu.

Protest gegen Präsident Donald Trump in New York
Picha: picture alliance/abaca/M. Elshamy

Zaidi ya wasafiri 100 wamekwama katika viwanja kadhaa vya ndege nchini Marekani. Makundi ya kutetea haki za binadamu na asasi za kiraia Marekani yaliandaa maandamano katika viwanja vya ndege kupinga agizo hilo la Trump na kuwasilisha kesi mahakamani kulipinga agizo hilo. Takriban watu 2,000 waliandamana katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa John F Kennedy.

Jaji wa mahakama kuu Ann Donnelly ametoa uamuzi Jumapili wa kupinga agizo la Rais la kuwazuia wasafiri kutoka nchi sita Syria, Somalia, Sudan, Libya, Yemen, Iran na Iraq kuingia Marekani kwa kuamuru wale walio na visa halali za kuingia Marekani wanastahili kuruhusiwa kuingia au kuendelea na safari zao.

Jaji Donnelly ameagiza serikali itoe orodha ya wale wote wanaozuiwa katika viwanja vya ndege  na kusema kuwarejesha katika mataifa yao kutokana na agizo la Rais, kunawaathiri vibaya. Maafisa wa usalama wa ndani na uhamiaji wamesema bado hawajaona agizo hilo la mahakama lakini wameahidi kuheshimu agizo hilo.

Trump autikisa ulimwengu

Agizo hilo la Trump lililotiwa saini siku ya Ijumma linasitisha mpango wa wakimbizi kwa siku 120 zijazo, kusitisha kutolewa kwa visa na kuzuiwa kwa wasafiri kutoka nchi kadhaa za Kiislamu kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Katika kipindi cha kampeini, Trump aliahidi kuchukua hatua za kukabiliana na kuongezeka kwa itikadi kali na kitisho cha ugaidi ili kuwalinda Wamarekani dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

Rais wa Marekani Donald Trump akitia saini agizoPicha: picture-alliance/Olivier Douliery/CNP/AdMedia

Hapo jana, kiongozi huyo wa Marekani alikanusha kuwa agizo hilo ni marufuku kwa Waislamu kuingia Marekani na badala yake kusema ni hatua ambazo muda wake umewadia na kwa sasa limeanza kutekelezwa vizuri kama inavyoshuhudiwa katika viwanja vya ndege.

Trump pia ameliagiza Jeshi la Marekani kuwasilisha mkakati mpya wa kupambana na IS katika kipindi cha siku thelathini zijazo. Wiki moja tangu kuingia madarakani, kiongozi huyo mpya wa Marekani ametia saini maagizo 18 ya Rais, mengi yao yakiutikisa ulimwengu na kuwaathiri mamilioni ya watu.

Hapo jana alifanya mazungumzo na viongozi watano wa dunia akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Waziri mkuu wa Australia Malcolm Turnbull.

Viongozi wa nchi za Kiislamu wameghadhabishwa na agizo hilo walilolitaja ya kudhalilisha na la kibaguzi. Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema muda umewadia wa kuondoa kuta badala ya kujenga kuta mpya. Wizara ya mambo ya nje ya Iran imedokeza huenda ikalazimika pia kuwazuia watalii kutoka Marekani kuizuru nchi hiyo.

Hata hivyo Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameunga mkono hatua ya Trump ya kujenga ukuta kati ya Marekani na Mexico akisema nchi yake ilifanya hivyo kati yake na Misri na matokeo yake yalikuwa mafanikio makubwa katika kuzuia mmiminiko wa wahamiaji kutoka Afrika. Kauli yake imeikera mno Mexico.

Viongozi wa Ulaya watiwa wasiwasi na hatua za Trump

Ufaransa, Ujerumani na Luxembourg zimesema zinatiwa wasiwasi na hatua hiyo ya Marekani. Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameuhimiza Umoja wa Ulaya kuungana na kutoa kauli kali kujibu hatua zinazochukuliwa na Rais Trump.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameshutumiwa vikali na wabunge mbalimbali nchini Uingereza, wakiwemo wa chama chake, kwa kutozungumzia dhidi ya kitendo cha Rais Donald Trump wa Marekani kuzuia wahamiaji.

Msemajii wa May amesema Waziri mkuu huyo mpya wa Uingereza hakubaliani na vizuzi vya wahamajia vilivyowekwa na Rais wa Marekani Donald Trump na kwamba ataingilia kati kama vitaathiri raia wa Uingereza.

Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau amendika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wakimbizi wanaokataliwa na Donald Trump, wanakaribishwa Canada bila ya kuangalia misingi ya dini zao.

Ujumbe uliotumwa kwa mashirika ya ndege kote duniani siku ya Jumamosi kutoka kwa chama cha usafiri wa ndege Marekani unasema marufuku hiyo ya wasafiri kutoka nchi saba za Kiislamu pia zinawahusu wahudumu wa ndege wanaotokea mataifa hayo licha ya kuwa na vibali vya usafiri, hawataruhusiwa kuingia Marekani.

Mashirika ya ndege kote duniani yakiwemo Emirates, Delta, KLM, shirika la Uingereza la British Airways, la Misri, Egypt Air na Qatar yanawazuia wasafari kutoka nchi zinazolengwa kutosafiri, kuwarejeshea nauli zao na kuwatahadharisha wasafiri kuhusu sera mpya za Marekani katika mitandao yao.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/ap

Mhariri: Mnette Sudi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW