1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ahadi ya Biden kuhusu utulivu kujaribiwa mjini Kenosha

3 Septemba 2020

Mgombea urais wa Marekani kupitia Democratic Joe Biden anakabiliwa na mtihani mkubwa wa ahadi yake ya kuwa kiongozi atakayeleta utulivu na atakayewaunganisha wamarekani katika taifa lenye mgawanyiko kwa kiasi kikubwa.

USA Präsidentschaftswahlen 2020 | Joe Biden in Pittsburgh
Picha: Reuters/A. Freed

Kenosha ni mji unaokabiliwa na msukosuko uliosababishwa na ubaguzi wa kimfumo na ziara ya mgombea huyo wa chama cha Democratic mwenye umri wa miaka 77 aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Marekani inajiri siku mbili baada ya mpinzani wake ambaye ni rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump kuutembelea mji huo. somaTrump kutembelea mji wa Kenosha licha ya kukataliwa

Joe Biden yeye anapanga kukutana na familia ya Jacob Blake ambaye bado yuko hospitali alikolazwa baada ya kupigwa risasi mara saba na askari polisi wa kizungu mgongoni pale askari hao walipojaribu kumkamata. Biden pia ana panga kujadiliana na jamii ya watu wa mji huo ikiwemo wafanyabiashara,viongozi wa kiraia na maafisa wa polisi.

Waandamanaji huko KenoshaPicha: Reuters/J. Vondruska

Mgombea huyo wa chama cha Democratic aliwaambia waandishi habari Jumatano kwamba hatua yake hiyo ni kwaajili ya kuhakikisha kwamba wanasonga mbele na wala hatowaambia watu wa Kenosha kitu gani wanachopaswa kufanya. Badala yake atawatia moyo kuzungumza kuhusu nini kinachopaswa kufanyika.

Ikiwa ni miezi miwili kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo ziara hii kwa Biden inaakisi mambo mawili kwa mgombea huyo; kwanza ni fursa lakini pili ni hatari ya kuitia kwenye majaribu ahadi yake ya kwamba anaweza kuliunganisha taifa, na kupata maridhiano hata pale ambapo hakuna uwezekano huo. Mwelekeo huo hapana shaka ni wa makusudi unaofanywa kumtofautisha na bwana Trump ambaye anapalilia migogoro.

Lakini migawanyiko imeongeza maandamano ya nchi nzima katika kipindi cha majira ya joto ingawa mengi ni maandamano ya amani lakini baadhi kama yale ya mjini Kenosha yaligeuka kuwa vurugu na uharibifu. Joe Biden ni Mmarekani mweupe aliyepata msukumo katika uteuzi wa chama cha Democratic kupitia kura za Wamarekani weusi.

Wito wa mageuzi makubwa

Tangu mwezi Mei 25 kilipotokea kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd aliyeuwawa na afisa wa polisi mzungu wa Minneapolis, Joe Biden amekuwa akitowa mwito wa kufanyika mageuzi makubwa katika mfumzo mzima wa polisi na kuitikia midahalo ya kitaifa juu ya suala la ubaguzi.

Mgombea wa Republican Donald Trump alipotembea Kenosha hivi karibuniPicha: Reuters/L. Mills

Na umuhimu juu ya yote hayo ni kwa Biden kumchagua seneta wa jimbo la Carlifonia Kamala Harris kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuwa mgombea mwenza kwa tiketi ya chama hicho cha Democratic.

Wakati huohuo Trump kwa upande wake akizijibu lawama za waandamanaji kwa kuwatetea polisi na kukanusha kwamba Wamarekani weusi wanakabiliwa na vizingiti ambapo wazungu haviwagusi.

Hatua ambayo bila shaka imekuwa ikilenga kuongeza nguvu msingi wake wa siasa za kuegemea upande wa watu weupe.

Trump alipokwenda Kenosha Jumanne alisisitiza juu ya kufuatwa sheria na taratibu na kuyatazama majengo yaliyoharibiwa lakini pia akajadiliana na maafisa wa polisi kuhusu njia za kuzima vurugu.

Rais huyo wa Marekani hajawahi kulishughulikia suala la ubaguzi au idara ya polisi nchini humo,badala yake amekuwa akidai kwamba Biden akitwaa urais ataleta vurugu na uharibifu katika miji ya Marekani.

 Chanzo:AP