1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AI: Matukio ya watu kunyongwa yapungua

12 Aprili 2018

Shirika la Amnesty International inasema kuwa kulikuwa na matukio machache ya adhabu ya kifo katika mwaka wa 2017 kuliko mwaka uliotangulia. Idadi ya watu waliohukumiwa kunyongwa duniani ilipungua pia

Indonesien Todesstrafe Portest
Picha: Getty Images/AFP/B. Ismoyo

Matukio ya kunyongwa watu yalipungua tena mwaka wa 2017, huku kukiwa na karibu 993 yaliyoorodheshwa katika nchi 23. Idadi hiyo ilipungua kwa asilimia 4 kutoka mwaka uliotangulia na chini kwa asilimia 39 kutoka mwaka wa 2015. Nchi 23 za kusini mwa jangwa la Sahara sasa zimeondoa adhabu ya kifo kwa makosa yote ya uhalifu. Ni nchi mbili tu za kanda hiyo, Somalia na Sudan Kusini, zilizotekeleza adhabu ya kifo mwaka jana.

Guinea ilifuta adhabu ya kifo kwa makosa yote ya uhalifu, wakati Kenya haitoi tena hukumu ya kifo iliyokuwa ya lazima kwa kosa la muaji. Burkina Faso imesifiwa na Amnesty kwa rasimu yake ya katiba ambayo inajumuisha kipengele cha kuondoa kabisa adhabu ya kifo, na Chad kwa kuanzisha sheria mpya ambayo inaruhusu tu hukumu ya aina hiyo katika kesi ya ugaidi.

Nchi zinazotekeleza hukumu ya kifo duniani

Katibu Mkuu wa Amnesty International Salil Shetty amesema uongozi wa mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara unatoa matumaini mapya kwamba adhabu hiyo ya unyama na ya kudhalilisha itaondolewa kabisa hivi karibuni. Takribani watu 2,591 walihukumiwa kifo katika nchi 53 mwaka jana, ikiwa ni idadi ya chini kutoka watu 3,117 iliyosajiliwa mwaka uliotangulia.

Takwimu hizo hazijumuishi matukio ya maelfu ya watu walionyongwa na kuhukumiwa kifo ambao Amnesty International inaamini yalitokea China, ambako yanazingatiwa kuwa siri ya serikali.

Ukiondoa China, asiimia 84 ya watu walionyongwa mwaka jana ilikuwa nchini Iran, Saudi Arabia, Iraq na Pakistan. Nchi zilizoanza tena kuwanyonga watu mwaka wa 2017 ni Bahrain, Jordan, Kuwait, na Umoja wa Falme za Kiarabu

Shetty amesema kuwa huku kukiwa na mafanikio barani Afrika, kutengwa kwa nchi zilizosalia duniani zinazowanyonga watu kunaonekana wazi. Hata miongoni mwa hizo nchi kuna hatua kadhaa zinazopigwa. Nchini Iran, matukio ya kutekelezwa adhabu ya kifo yalipungua kwa asilimia 11 na idadi ya watu walionyongwa kutokana na kesi za dawaza kulevya ikapungua hadi asilimia 40.

China inaongoza duniani katika kuwanyonga watuPicha: picture-alliance/AP Photo

Lakini Amnesty International imesema inasikitisha kuwa utekelezaji wa adhabu ya kido unaendelea kufanywa kwa kesi zinazohusiana na dawaza kulevya, huku nchi 15 mwaka jana zikitangaza hukumu za kifo au kutekeleza hukumu hizo.

Matukio ya kunyongwa yanayohusiana na dawa za kulevya yalitokea China, Iran, Singapore na Saudi Arabia, ambako watu walionyongwa kuhusiana na dawa za kulevya waliongezeka kutoka asilimia 16 ya jumla ya matukio hayo katika mwaka wa 2016 hadi asilimia 20 katika mwaka wa 2017.

Shirika hilo la haki za binaadamu pia limeelezea wasiwasi kuwa karibu watu watanon nchini Iran walinyongwa mwaka jana kwa uhalifu uliofanywa wakati wakiwa chini ya umri wa miaka 18, huku watu wengine 80 wenye hali kama hiyo wakisubiri kunyongwa.

Watu wenye mattaizo ya kiakili au ulemavu wa kiakili walinyongwa au wanakabiliwa na hukumu ya kifo nchini Marekani, Japan, Pakistan, Singapore na Maldives. Amnesty international imesema sasa ni wakati wa kuweka shinikizo la kutaka adhabu ya kifo iondolewe.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusra Buwayhid