1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AI: Misri yakabiliwa na mateso makubwa

16 Aprili 2018

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International limesema hali ya mateso nchini Misri ni mbaya zaidi chini ya utawala wa rais Abdel Fattah al-Sisi kuliko wakati mwengine wowote.

Aida Seif el-Dawla Mitbegründerin des Nadeem-Zentrums für Folteropfer in Kairo
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. El Raai

Kituo cha kupambana na utesaji wa watu cha Nadeem kinawashughulikia wahanga wa machafuko na mateso hayo mjini Cairo ndicho kitapokea tuzo ya Kimataifa ya shirika la Amnesty inayotolewa Ujerumani kila baada ya miaka miwili. Hafla ya kutolewa kwa tuzo hiyo itafanyika Jumatatu mjini Berlin.

Shirika la Amnesty limetangaza kwamba linataka kuwaunga mkono watu wote wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu nchini Misri kupambana na hatari ya mateso na machafuko.

Kituo cha Nadeem kinaripotiwa kuwa kituo cha pekee nchini Misri ambacho kinawashughulikia watu wanaopitia kadhia hiyo. Kwa zaidi ya miaka 20 Kituo hicho kimekuwa kikinakili mateso yanayofanywa na vikosi vya usalama vya Misri.

Hakujawa na wakati ambapo mateso na machafuko yalikosa utu kama ilivyokuwa mwaka 2013

Katika taarifa yake, Amnesty International imesema wafanyakazi wa kituo hicho wamekuwa wakitoa misaada ya kimatibabu na kisaikolojia kwa wahanga wa mateso na wamekuwa wakiweka wazi ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu unaoendelea.

Mwanaharakati wa Kituo cha Nadeem Aida Seif el Dawla, wa pili kutoka kulia Picha: picture-alliance/dpa/Polaris Image/D. Smilie

Aida Seif al-Dawla ni mwanzilishi mwenza wa kituo hicho.

"Hakujawa na wakati ambapo mateso na machafuko yalikosa utu kama ilivyokuwa mwaka 2013. Tulichokiona tangu mwaka 2013 ni mambo ambayo hata hayafikiriki, hayawezi kuelezeka, ni machafuko kwa machafuko na unyama kwa unyama," alisema Aida. "Kawaida inaanza na kipigo, kipigo cha aina yoyote kupigwa mateke na makofi na ni jambo ambalo linafanyika kila wakati mpaka limezoeleka mpaka watu hawalizungumzii tena. Kisha baada ya hapo unatumika umeme katika ulimi, vidole vya miguuni na hata sehemu za siri," aliongeza Aida.

Tangu mwaka 2016 uongozi nchini Misri umekuwa ukikishambulia Kituo hicho ambacho kliniki yake ilifungwa Februari mwaka jana na kituo hicho kikakata rufaa.

Tuzo hiyo inatolewa kila baada ya miaka miwili

Katibu Mkuu wa Amnesty International tawi la Ujerumani Markus Beeko amesema kwamba serikali ya Rais Abdel Fattah al-Sisi ina mpango maalum wa kuwanyamazisha wapinzani wa kisiasa. Na kuhusiana na hilo la wanasiasa wapinzani Aida anasema wao pia huteswa mno.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ametuhumiwa kwa matesoPicha: Reuters/Y. Kourtoglou

"Na kwa wafungwa wa kisiasa kuna kitendo cha kufungwa macho kwa kitambaa ambacho kinaanza siku mtu atakapokamatwa na kinaendelea kwa siku zote watakazokuwa chini ya ulinzi wa serikali," alisema Aida. "Wakiwa wamefungwa macho hawajui tofauti kati ya usiku na mchana na hawakubaliwi kuzungumza na watu wengine waliokamatwa pamoja nao," aliongeza Muasisi huyo wa Kituo cha Nadeem.

Kila baada ya miaka miwili Shirika la Amnesty la Ujerumani linawatuza watu binafsi na mashirika yanayofanya kazi za kutetea haki za binadamu katika mazingira magumu. Lengo la tuzo hii ni kutambua dhamira ya watu hawa, kuwaunga mkono katika yale wanayofanya na kuhakikisha kwamba kazi yao inatambulika.

Mwaka2014 Alice Nkom kutoka Cameroon ndiye aliyetuzwa na miaka miwili baadae mwaka 2016 Henri Tiphagne kutoka India ndiye aliyekuwa mshindi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPD/Tableau

Mhariri: Gakuba Daniel