1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aina mpya ya kirusi cha Covid-19 yapewa jina la Omicron

Sylvia Mwehozi
27 Novemba 2021

Shirika la afya ulimwenguni WHO limekitangaza kirusi kipya cha B.1.1.529, kilichogundulika hivi karibuni nchini Afrika Kusini kuwa chenye kutia wasiwasi na kukiita jina la Omicron.

USA | Coronavirus Variante SARS-CoV-2
Picha: NIAID-RML/AP/dpa/picture alliance

Uainishaji huo unakiweka kirusi cha Omicron katika kipengele cha aina ya kirusi cha Covid-19 kinachosumbua zaidi, pamoja na kile cha Delta ambacho kimeenea ulimwenguni, pamoja na vile vya Alpha, Beta na Gamma.

WHO imesema itachukua wiki kadhaa kukamilisha utafiti juu ya Omicron na kuona ikiwa kuna mabadiliko yoyote katika maambukizi, ukali au athari katika chanjo za Covid-19, vipimo na matibabu yake. Ukiacha Afrika Kusini, kirusi cha Omicron kimepatikana pia katika nchi za Israel, Botswana, Ubelgiji na Hong Kong.

Mataifa kadhaa yafuta safari za ndege

Mataifa kadhaa ulimwenguni yaliharakisha katika kufuta safari za ndege ili kupunguza kasi ya maambukizi ya Omicron siku ya Ijumaa, wakati masoko ya hisa na bei za mafuta vikishikwa na mtikisoko kutokana na aina hiyo mpya ya kirusi kinachohofiwa kuleta athari katika uchumi wa dunia ambao ulikuwa umeanza taratibu kuimarika.

Abiria katika uwana wa ndege wa Heathrow, LondonPicha: Leon Neal/Getty Images

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kusitisha safari za ndege za abiria kutoka mataifa saba ya kusini mwa Afrika, ili kuzuia kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha corona. Mapema siku ya Ijumaa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza hatua za dharura katika sheria za kusafiri miongoni mwa nchi wanachama.

Nchi zilizokumbwa na marufuku hiyo ni pamoja na Botswana, Eswatini, Lesotho, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe. Wasafiri wanaowasili kutoka nchi hizo saba watalazimika kukaa karantini na kufanya vipimo vya corona. Mataifa mengine ikiwemo Marekani pia nayo yamesitisha safari za ndege kutoka mataifa hayo saba. Wakati huo huo Gavana wa New York Kathy Hochul ametangaza hali ya dharura kuanzia tarehe 3 Desemba hadi Januari 15.

Wizara ya afya ya Afrika Kusini hata hivyo imeushambulia ulimwengu kwa kutangaza marufuku ya safari za ndege ikisema hatua hiyo ni ya kibabe, na " isiyo ya kisayansi na kinyume na ushauri wa WHO". Kirusi hicho kinaelezwa kuchochea ongezeko la maambukizi ya Covid-19 nchini humo.

Waziri wa afya wa Afrika Kusini Joe Phaahla amesema mwelekeo huo haukuwa sahihi akiongeza kuwa baadhi ya watawala wanajaribu kumtafuta wa kumvika kengele katika tatizo linaloushughulisha ulimwengu.

Vyanzo: afp/dpa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW