Ajali mbaya kabisa ya treni katika historia ya binadamu katika Korea ya Kaskazini
23 Aprili 2004Baada ya kunyamaza kimya kwa muda wa masaa 24, Korea ya kaskazini sasa imethibitisha ajali mbaya kabisa katika historia ya mgongano wa treni mbili iliyotokea nchini humo. Serikali mjini Pjöngjang, imekiomba chama cha msalaba mwekundu kuwahudumia wahanga walionusurika ajali hiyo. Mwakilishi wa chama hicho John Sparrow, amesema watumishi wake tayari wako njiani kuelekea mahali ajali hiyo ilitokea katika mji wa mpakani kuelekea China wa Ryongchom.
Baada ya mgongano wa treni hizo mbili za kusafirisha kemikali ulitokea mripuko mkubwa ambao unasemekana uligharimu roho za watu si chini ya
3,ooo na wengine wengi kujeruhiwa. Lakini kulingana na taarifa za hadi sasa, idadi ya wahanga wa ajali hiyo bado haijulikani kwa hakika, hasa mtazamaji akiona picha za setelite zilizotangazwa na Marekani masaa 18 baada ya msiba huo, zinazoonyesha moshi mweusi kutoka mripuko huo juu ya mji huo wa mpakani. Picha hizo za jana zinaonyesha kwamba, moto uliotokea baada ya treni hizo mbili kugongana, bado haujazimwa kamili.
Korea ya kaskazini ni nchi inayojulikana hupendelea kuendesha mambo yanayoihusu kwa siri kubwa. Hata kuhusiana na ajali hii mbaya kabisa ya treni katika historia ya mwanadamu habari zinazohusika zinachunjwa na serikali. Kwa sababu hii, chanzo cha ripoti zote kuhusiana na ajali hiyo, zinatokana na mashahidi wanaoishi katika upande wa China na kutokana na idara za upelelezi za korea ya kaskazini.
Baada ya mripuko huo ulioteketeza kabisa stesheni ya treni ya mji huo wa mpakani, ilianza kunyesha mvua ya vipande vya chuma kutoka hewani, vilivyorushwa hadi katika mji wa jirani wa Sinuju, ulioko kiasi ya kilometa 15 kutoka mahali pa ajali.
Idadi hii ya wahanga 3 000 waliouliwa au kujeruhiwa, ni makisio tu, kwa sababu mripuko huo katika stesheni hiyo muhimu ya usafirishaji shehena, hapana shaka umegharimu roho za wahanga zaidi. Gazeti moja la Korea ya Kaskaini linaripoti kwamba, majeruhi wa ajali hiyo, wanapelekwa kwa ajili ya matibabu katika mji wa mpaka kuelekea China wa Dang-dong. Hii inamaanisha idara za huduma za afya za Korea ya Kaskazini, hazina uwezo wa kuchukua hatua za dharura katika msiba huo. Inasemekana wengi miongoni mwa majeruhi, hawana nafasi ya kuokoka mripuko huo.
Katika Korea ya Kaskazini zinazagaa fununu kwamba, mripuko huo wa jana ulikuwa ni jaribio ambalo halikufanikiwa, la kumuua kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Il, wakati wa kurejea nyumbani kwa njia ya reli kutoka ziarani nchini China. Sababu ni kwa kuwa, ajali hiyo ilitokea masaa tisa tu baada ya dikteta huyo kuvuka mpaka akitokea mjini Beijing. Pia inasemekana Kim Jong Il alivunja mpango wake wa kusita katika mji wa jirani wa Sinuju, lakini watumishi wa idara ya upelelezi mjini Seoul, wana shaka shaka kama ajali hiyo kwa kweli ilikuwa imepangwa kumuua kiongozi wa nchi hiyo.
Inamshangaza mtu kuhusu ajali hiyo, kwa sababu kikawaida wakati Kim Jong Il anapofanya safari nchini, usafiri wa kila aina popote pale anapoelekea huwa unapigwa marufuku kwa sababu za usalama wake. Ndio maana wadadisi wanasema, huenda ajali ya mripoko huo ilisababishwa na makosa ya waendeshaji au teknolojia za treni hizo mbili.