1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Akufo-Addo wa Ghana aapishwa kwa muhula mwingine madarakani

Sylvia Mwehozi
7 Januari 2021

Rais Nana Akufo-Addo, ambaye alichaguliwa tena kwa ushindi mwembamba mnamo Desemba 7, ameapishwa hivi leo kwa muhula mwingine madarakani wakati bunge likitawaliwa na ghasia.

Ghana Accra Präsident Nana Akufo-Addo
Picha: picture-alliance/AP Photo

"Mimi, Nana Addo Dankwa Akufo Addo, naapa kwa jina la mwenyezi Mungu kwamba nitaonyesha imani ya kweli na utii kwa Jamhuri ya Ghana kwa mujibu wa sheria, kwamba nitasimamia enzi na uadilifu wa Ghana, kwamba nitahifadhi, nitalinda na kutetea katiba ya Jamhuri ya Ghana, eeh Mungu nisaidie", aliapa Akufo-Addo hii leo. 

Wanajeshi wa Ghana wamelazimika kuvamia bunge ili kutuliza makabiliano yaliyozuka baina ya vyama pinzani katika vurugu za usiku wa kuamkia Alhamis kuelekea kuapishwa kwa wabunge. Vurugu zilizuka baada ya mbunge mmoja kutoka chama tawala kujaribu kukwapua sanduku la kura wakati wa zoezi la kumchagua spika wa bunge.

Vurugu hizo zilidumu kwa masaa kadhaa kabla ya wanajeshi kuwasili, huku televisheni ya taifa ikionyesha tukio zima. "Kulikuwa na ukiukwaji kamili wa sheria na kanuni", alisema mbunge mteule Kwame Twumasi Ampofo wa chama cha upinzani cha National Democratic Congress NDC. Bunge jipya limegawanyika katikati ya vyama viwili vikuu, na kutoa kitisho cha mkwamo wa kushughulikia matatizo ya Ghana.

Jengo la bunge la Ghana mjini AccraPicha: DW/I. Kaledzi

Ghana inachukuliwa kuwa nchi iliyokamaa kidemokrasia katika eneo lenye machafuko la Afrika Magharibi, ingawa uchaguzi wa mwaka jana uligubikwa na madai ya udanganyifu kwa mujibu wa upinzani huku watu watano wakipoteza maisha. Waangalizi wote wa ndani na wa nje walisema kwa ujumla uchaguzi ulikuwa huru na haki, ingawa ufanisi wa tume ya uchaguzi bado umetiliwa mashaka. Wabunge kadhaa wa upinzani walishatakiwa kwa kufanya mikusanyiko kinyume na sheria siku ya Jumatatu baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Picha za vidio za makabiliano ya usiku katika bunge zimeonyesha baadhi ya wabunge wakitupiana maneno na ugomvi mkali na wapinzani wao. Chama tawala cha New Patriotic Party NPP kilishinda viti 137 katika bunge lenye wabunge 257 baada ya kupoteza viti 32 katika uchaguzi na kufanya chama cha NDC nacho kudhibiti viti sawa 137. Hata hivyo Mbunge mmoja wa upinzani alisimamishwa kazi jana kutokana na kuwa na uraia wa nchi mbili na hivyo kusababisha viti vya wapinzani kupungua na kufikai 136.

Taifa hilo lenye wakaazi milioni 30 lililoathiriwa vibaya na janga la COVID-19 linatarajiwa kushuhudia uchumi wake ukikua kwa asilimia ndogo mwaka huu katika kipindi cha miongo mitatu kwa hadi asilimia 0.9 kulingana na shirika la fedha ulimwenguni IMF kutoka asilimia 6.5 mwaka 2019. Serikali pia inakabiliwa na kibarua cha kujinasua kwenye mzigo wa madeni ambao unazidi kuongezeka na kuvuka asilimia 70 ya pato la taifa mnamo mwezi Septemba.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW