Al Ahly wabeba ubingwa wa Afrika kwa mara ya 11
12 Juni 2023Beki Mohamed Abdelmonem alisawazisha kwa njia ya kichwa jana usiku na kulazimisha sare ya 1 -1 ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco na kuwapa ubingwa huo. Bao lake lilifuta lile lililofungwa na Yahia Attiyat Allah lililokuwa limewaweka kifua mbele mabingwa hao watetezi na kuipa timu hiyo ya Cairo ushindi wa jumla ya 3-2 baada ya ushindi wa 2 -1 katika mkondo wa kwanza siku saba zilizopita.
Tofauti na Ulaya, mabao ya ugenini yanahesabika kama mawili katika mashindano ya vilabu Afrika wakati timu zinapomaliza mechi kwa sare baada ya mikondo miwili, na Wydad ingebaki na Kombe kama wangeshinda 1 – 0.
Ahly ilitia kibindoni dola milioni nne kwa kushinda na Marcel Koller akawa kocha wa kwanza Mswisi kushinda taji hilo kubwa la vilabu Afrika.
Ulikuwa ushindi wa tatu wa Ligi ya Mabingwa katika misimu minne kwa Ahly baada ya kuwabwaga Wamisri wenzao Zamalek mwaka wa 2020 na Kaizer Chiefs wa Afrika Kusini mwaka uliofuata.
afp