Al-Bakr alionesha dalili za itikadi kali
15 Oktoba 2016Aliweka video za kijihadi mtandaoni wakati akiwa nchini Ujerumani, kabla ya kusafiri mapema mwaka huu na kuelekea nchini Syria katika mji wa Idlib, unaodhibitiwa na wanamgambo wa itikadi kali za kidini amesema kaka huyo. Alaa al-Bakr ameiambia Reuters kupitia njia ya simu kwamba ndugu yake alimwambia alikwenda Syria pamoja na waokozi wa kujitolea wa nyakati za dharura, lakini Alaa anaamini alibadilishwa na maimam wa mji mkuu wa Ujerumani Berlin kwa kumjaza mitazamo ya itikadi kali za kidini pamoja na kumshawishi kurudi nchi aliyotokea ya Syria na kujitolea kwa jina la jihadi.
"Hiyo ndiyo sababu tunayoamini ilimrudisha nchini Syria," Alaa ameliambia shirika hilo la Reuters akiwa katika kijiji cha Sa´sa kusini magharibi mwa mji mkuu wa Syria wa Damascus. "Miezi saba iliyopita alikwenda Uturuki na katika safari hiyo alitumia miezi miwili nchini Syria. Alitupigia simu na kutuambia amejiunga na kikosi cha waokozi wa kujitolea mjini Idlib, wanaojulikana kwa kuvaa helmeti nyeupe."
Idlib, ni mji ulio karibu na mpaka wa Uturuki, na jimbo lenye jina hilo hilo la Idlib ni ngome kuu ya makundi ya wanamgambo ikiwa ni pamoja na kundi la Jabhat Fateh al-Sham, ambalo liliwahi kuwa na uhusiano na makundi ya al-Qaeda pamoja na al-Nusra Front.
Alaa amesema Jaber ambaye alikuwa anaishi kisheria kama mkimbizi nchini Ujerumani na kujiua baada ya kukamatwa na polisi kwa shutuma za kupanga shambulizi la bomu katika uwanja wa ndege mjini Berlin, alikuwa ni muumini wa Kiislamu mwenye nia ya kuendelea na masomo kwa kujiandikisha chuo kikuu nchini humo.
Jaber, mwenye umri wa miaka 22 aliwakwepa polisi walipolivamia jengo alimokuwa akiishi mjini Chemnitz na kukuta vifaa vya kulipua katika chumba chake, lakini baadae alikamatwa na wakimbizi wenzake wa Kisyria na kukabidhiwa kwa polisi baada ya kumfunga kamba katika chumbao chao mjini Leipzig.
Kansela Merkel ataka kufanyike uchunguzi huru
Gazeti la kila wiki la Ujerumani la "Welt am Sonntag" limeripoti kuwa maafisa wa kijasusi wa Marekani waliwataarifu wenzao wa Ujerumani kwamba walinasa mawasiliano kadhaa ya simu kati ya Jaber na mtu mmoja wa kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS, la nchini Syria.
Katika mawasiliano hayo, Jaber al-Bakr ameripotiwa kujadili na mwanamgambo wa IS njama za kufanya shambulizi la kigaidi, ambazo maafisa wa Ujerumani wanasema ni pamoja na kuushambulia uwanja wa ndege wa mjini Berlin. Al-Bakr alijiunga na kundi la IS nchini Syria mnamo Septemba 2015, kwa mujibu wa ripoti za maafisa wa Ujerumani.
Kansela, Angela Merkel, wa Ujerumani ameamuru kufanyike uchunguzi juu ya kujiua kwa al-Bakr kufuatia sakata la kisiasa lililozuka baada ya kifo chake. Mtu anapojiua akiwa ameshikiliwa jela "basi kuna kitu kilikwenda vibaya, na dalili za onyo hazikutambuliwa," amesema msemaji mkuu wa Merkel, Steffen Seibert. Wito wa Merkel wa kufanyika uchunguzi wa kujiua kwa mahabusu huyo, kunaweza kuleta mvutano na mshirika wake wa chama chake cha kihafidhina - mkuu wa jimbo la Saxony la Ujerumani mashariki, Stanislaw Tillich - aliyepinga vikali kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu tukio hilo.
Uchunguzi wa maiti umethibitisha kwamba al-Bakr alijinyonga kwa kujitundika katika vyuma vya chumba cha mahabusu na kwa kutumia shati lake alilokuwa amevaa. Na Tillich alikubali Ijumaa kwamba kulitendeka makosa yaliyoruhusu kifo hicho kutokea.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa shirikisho imesema kuwa al-Bakr alikataa kutoa tamko lolote lile baada ya mahojiano yake ya kwanza na polisi pamoja na kuhojiwa na hakimu wa Dresden, mji mkuu wa jimbo la Saxony.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere amesisitiza kwamba "kwa wale wanaowajibika na tukio hili wanajua kuna kazi kubwa ya kufanywa mbele yao" ya kufichuwa habari zaidi juu ya njama zinazoshukiwa za kutega bomu mjini Berlin.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpa/rtre
Mhariri: Bruce Amani