Al Hilal yatoka sare na St Éloi Lupopo
1 Desemba 2025
Al Hilal, ambayo kwa sasa inacheza mechi zake nchini Rwanda, ilimkosa winga wake nyota Jean Claude Girumugisha aliyesimamishwa na CAF kwa mechi tatu kufuatia utovu wa nidhamu katika ushindi wa 2-1 dhidi ya MC Alger mnamo Novemba 21 kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.
Shirikisho la Soka Afrika, CAF limemtoza Girumugisha faini ya dola elfu tano na pia kuipiga Al Hilal faini ya dola elfu kumi na tano kutokana na tukio hilo. Kwa sasa, Al Hilal inashika nafasi ya pili katika Kundi C pamoja na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na St Éloi Lupopo ya DR Congo.
Mgogoro wa Uongozi Rayon Sports
Wakati hayo yakijiri, klabu ya Rayon Sports imekumbwa na mvutano wa kiutawala. Wiki iliyopita, Bodi ya Uongozi ya Rwanda (RGB) iliitisha mkutano uliowahusisha viongozi wa RGB na wajumbe 18 wa kamati mbalimbali za Rayon Sports.
Changamoto zilizobainika si mara ya kwanza kutokea, zikiwemo matatizo ya uongozi. Uongozi huo usio thabiti, ndio umeifanya timu hiyo kutoonekana kwenye kiwango kizuri na kushindwa kuwapa burudani mashabiki.
Kazaire Judith, Mkuu wa Idara ya Mashirika ya Kiraia na Vyama vya Siasa katika RGB, alisema:
"Katika vyombo vya habari kumekuwa na maneno ya kushtumiana, mambo ambayo hayafai katika uongozi wa klabu. Ndiyo sababu RGB pamoja na viongozi wote wa Rayon Sports wameamua kuitisha mkutano ili tujadili changamoto zinazoikabili timu.”
Mkutano huo uliamua kuvunja kamati zote zilizokuwa zikiongoza Rayon Sports na kuunda Kamati ya Mpito inayoongozwa na AL Hadji Murenzi Abdallah. Wajumbe wengine ni Musabyimana Jean Baptiste, Gakwaya Olivier, Akayezu Josée na Nubumwe Jean Bosco. Kamati hiyo imepewa miezi mitatu kuanzia Novemba 25, 2025, ili kupitia na kuboresha kanuni na taratibu za Rayon Sports pamoja na kuweka mfumo mpya wa uongozi.
Shabiki mmoja wa Rayon Sports kutoka Muhanga alieleza hisia zake:
"Tunastahili ubingwa… Mashabiki ni mchezaji wa 12. Rayon Sports inahitaji sapoti tu, haihitaji mambo mengi.”