Al Jazeera yaanika 'Nyaraka za Palestina'
24 Januari 2011Baada ya WikiLeaks, sasa ni hiki kinaweza kuitwa 'JazeeraLeaks.' Jana usiku (23 Januari 2011) kituo cha televisheni cha Al Jazeera, likitangaza rasmi uwekwaji hadharani wa karibuni nyaraka 17,000 ambazo kituo hicho kinasema kwamba, zimetoka katika vyanzo vya uhakika.
Nyaraka hizi zinatoa siri ya kile kilichokuwa kikizungumzwa ndani ya kuta nne, baina ya wajumbe wa upatanishi wa Kipalestina, wa Kiisraeli na wa Kimarekani; kubwa zaidi ikiwa ni wajumbe wa Kipalestina, wakiongozwa na Saeeb Erakat, kukubali kuyatoa au kuyahalalisha maeneo nyeti sana ya ardhi ya Palestina kwa Israel, kama vile eneo zima la Jerusalem ya Mashariki, ukiacha sehemu ndogo tu iitwayo Jabal Abu Ghneim.
Mtangazaji wa Al Jazeera, Adrian Finnegan, anasema haijawahi kutokea kwenye historia ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, kiwango kikubwa cha siri za ndani kama hiki kuwekwa hadharani.
"Nyaraka za Palsetina zina taarifa nyingi zaidi kuweza kupenya katika historia ya mgogoro wa Israel na Palestina." Anasema Finnegan.
Utangazaji na uchapishwaji wa nyaraka hizi, ambazo tayari zimeanza kuwekwa kwenye mtadao wa Al-Jazeera tangu jana usiku, una athari kubwa sana kwa heshima ya viongozi wa chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO).
Viongozi wa kundi la Fatah, kama Rais Mahmoud Abbas, ambalo ni sehemu ya PLO na ndilo linaloongoza Mamlaka ya Ndani ya Palestina, wamekuwa kila siku wakijidhihirisha kama watetezi wakubwa na wa pekee wa ardhi ya Palestina, kwa gharama ya kuyatenga makundi mengine kama vile Hamas.
Tayari maafisa wa mamlaka hiyo wameuhoji uhalali wa nyaraka hizi wakisema kwamba ni za uongo na au zinasema nusu ukweli. Katika mahojiano na gazeti la kila siku la al-Ayyaam la nchini Misri hii leo, Saeeb Erakat alisema kwamba utolewaji wa taarifa kama hizi na katika wakati kama huu ni njama ya makusudi ya kuwaharibia viongozi wa Kipalestina taswira yao kwa jamii.
Miongoni mwa yale yaliyomo kwenye nyaraka hizi, ni dondoo za video za kikao cha tarehe 15 Juni 2008 kati ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani , Condoleezza Rice, waziri wa Mambo ya Nje na mjumbe wa Israel katika mazungumzo hayo, Tzipi Livni, waziri mkuu wa zamani wa Palestina, Ahmed Qureia na mkuu wa wajumbe wa upatanishi wa Palestina, Saeeb Erakat, ambapo Qureia anaonekana akipendekea utanuliwaji wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo lote la Jerusalem ya Mashariki.
Lakini kwa mujibu wa nyaraka hizo, ni Erakat ndiye aliyekwenda umbali wa kutaja orodha ya maeneo ambayo Mamlaka ya Palestina ilikuwa tayari kuyatoa sadaka, yakiwemo ya Ramat Alon, Ramat Shlomo, Gilo na Talpiot.
Mwandishi wa gazeti la The Guardian la Uingereza, ambalo nalo limeanza kuzichapisha nyaraka hizo, Seumas Milne, anasema kwamba nyaraka hizi zinaonesha sura halisi ya wajumbe wa Kipalestina wanapokuwa kwenye meza za majadiliano, ikiwa na tafauti sana na kile wanachokionesha wakiwa kwenye majukwaa ya kisiasa:
"Nyaraka hizi zinaonesha pia picha ya udhaifu na fadhaa kwa upande wa Palestina katika mazungumzo ya upatanishi, kwamba hawajapiga hatua yoyote ile." Anasema Milne.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman