Al-Qaeda kuanzisha tawi India
4 Septemba 2014Tangazo la Al-Qaida limetolewa kwa njia ya video iliowekwa mtandaoni. Katika video hiyo ya dakika 55, kiongozi wa Al-Qaida, Ayman al- Zawahri anatoa maelezo ya kina kuhusu nia yake ya kufungua tawi nchini India. Al-Zawahri amewataka waislamu wafanye vita dhidi ya wale aliowaita maadui.
Wataalamu wa kupambana na ugaidi wameeleza kwamba wanaamini kuwa video ya Al-Zawahri ni halisi. Kwa sababu hiyo serikali ya India imevitaka vyombo vyote vya usalama kuwa katika hali ya tahadhari.
Serikali yasema imejiandaa
Akiuzungumzia uwezekano wa al-Qaida kufungua tawi nchini India, mmoja wa viongozi wa chama tawala cha BJP Sabmit Patra amesema: "Suala hili ni kubwa na linatupa wasiwasi. Lakini tuna serikali yenye nguvu. Serikali yetu itachukua hatua madhubuti na haitaruhusu jambo hili kutokea."
Katika ujumbe wake wa video, Al-Zawahri ametaja maeneo kadhaa ya India, likiwemo jimbo la Gujarat anakotokea waziri mkuu Narendra Modi. Inaaminika kwamba al-Qaeda anataka kulipiza kisasi kwa Modi kwani yeye alikuwa waziri wa mambo ya ndani mwaka 2002 wakati ambapo migogoro ya kidini ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000. Wengi wao walikuwa waislamu.
Sehemu kubwa ya raia bilioni 1.2 wa India ni Wahindu. Hata hivyo, idadi ya waislamu inafikia milioni 175 na hivyo kuifanya India moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na waislamu wengi duniani.
Upinzani na Dola la Kiislamu
Mtaalamu wa masuala ya usalama kutoka India, Alok Bansal ametahadharisha kwamba tishio la al-Qaida lazima lipewe uzito. "Mashirika ya kijasusi ya India yanapaswa kuchukua hatua kupambana na al-Qaida kwa sababu majimbo ambayo al-Qaida yameyazungumzia waliongelea maeneo kama Gujarat na pia Khorasan," alisema Bansal. "Lazima tuelewe hilo na tuchukue hatua tukikumbuka kwamba hili ni suala nyeti sana."
Ingawa serikali ya India inawahakikishia raia wake kwamba imejiandaa, haijasema imechukua hatua gani za ziada kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya al-Qaida. Mpaka sasa hakuna ushahidi kwamba al-Qaida imeshaingia India. Wataalamu wanaamini kwamba kundi hilo limeuchagua wakati huu kupanua eneo lake kwa sababu kundi pinzani la Dola la Kisslamu nalo linaendelea kuteka maeneo huko Iraq na Syria.
Mwanidishi: Elizabeth Shoo/dpa/reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga