Al Shabaab wadai kufanya mauaji mengine Kenya
2 Desemba 2014Wawili kati ya wafanyakazi 36 waliouwawa, walikatwa vichwa katika eneo ambapo wanamgambo hao waliliteka nyara basi moja na kuwauwa kwa kuwapiga risasi vichwani watu takriban 28 wiki iliyopita.
Katika kisa cha leo Jumanne (02.12.2014) Wapiganaji hao waliwavamia mamia ya wafanyakazi walipokuwa wamelala katika makambi yao karibu na eneo la kuchimba mawe, kwenye kaunti ya Mandera karibu na mpaka wa Kenya na Somalia mwendo wa saa saba usiku, alisema mkuu wa kijiji cha Korome kilicho karibu na eneo lililoshambuliwa.
"Wanamgambo hao waliwatenga waislamu na wakristo, kisha wakawaambia wakristo wote walale chini na kuwapiga risasi kichwani," alisema mkuu huyo wa kijiji cha Korome Hassan Duba.
Kulingana na Peter Nderitu, mfanyakazi katika katika eneo hilo la kuchimba mawe, wapiganaji zaidi ya 50 walifika hapo na kupiga risasi hewani, baada ya kusikia milio ya risasi, Nderitu aliamka mbio na kujificha katika handaki moja ambapo aliwasikia wenzake wakiulizwa kutoa shahada, neno linalotamkwa na waumini wa kiislamu kushahidia kuwa mungu ni mmoja. Baada ya hapo akasikia milio mingine ya risasi.
Peter Nderitu, ameendelea kusema kwamba alitoka katika eneo alilojificha saa mbili baada ya tukio hilo na ndipo alipoona miili ya wenzake ikiwa katika mistari miwili na karibu wote walipigwa risasi kichwani.
Serikali ya Kenya imesema imeanzisha uchunguzi juu ya kisa hicho
Huku hayo yakiarifiwa Serikali ya Kenya imethibitisha kuuwawa kwa watu hao 36 huku ikisema imeanzisha uchunguzi juu ya kisa hicho.
Hata hivyo wakosoaji wanasema serikai hiyo ya Uhuru Kenyatta mpaka sasa haijajikakamua vilivyo kuhakikisha usalama wa wakenya, tangu wanamgambo wa al shabaab walipolishambulia jumba la biashara la Westgate mjini Nairobi mwaka uliopita na kusababisha vifo vya watu 67.
Kundi hilo la wanamgambo limekuwa likisema mara kwa mara kwamba linafanya mashambulizi ili kuiadhibu serikali ya Kenya kwa kutuma wanajeshi wake kujiunga na wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaojaribu kulidhibiti kundi hilo nchini Somalia.
Msemaji wa Al Shabaab Ali Mohamud Rage amesema hawana huruma kwa watu wasioamini, na watafanya kila wawezalo kuwalinda waislamu wanaoteseka kutokana na mateso na kunyanyaswa wanayodai kufanywa na serikali ya Kenya.
Wakati huo huo wapinzani wa serikali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki wanasema hatua ya kuwepo kwa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia hakujawahakikishia wakenya usalama wao na kutaka wanajeshi hao waondolewe.
"Walipaswa kuwa na eneo lisilokuwa na shughuli za kijeshi kati ya nchi yetu na eneo lililo na vurugu upande mwengine wa Somalia, lakini mpaka sasa hawajafabnya hivyo, kwa hivyo tunasema ondokeni," alisema Dennis Onyango, msemaji wa upande wa upinzani unaoongozwa na mwanasiasa Waziri Mkuu wa Zamani nchini Kenya raila Odinga.
Mauaji hayo yametokea wakati ambapo mjadala kuhusu hali ya usalama nchini umepamba moto.
Chama kikuu cha Upinzani ODM kimemtaka Rais Uhuru Kenyatta kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza jukumu lake la kuwahakikishia wakenya usalama.
“Ofisi ya Rais ni kubwa kuiliko raia yeyote na ni ofisi inayotazamwa kwa heshima na raia. ikiwa Rais Kenyatta ameona kwamba kazi hiyo ni kubwa kumshinda au akiona haimridhishi basi ajiuzulu” alisema Katibu Mkuu wa chama cha ODM Anyang' Nyong'o.
Huku hayo yakiarifiwa kufuatia mauaji watu 28 siku kumi zilizopita serikali ilitoa onyo kali kwa kundi la Al-Shabaab lililodai kutekeleza mauaji hayo, Makamu wa rais William Ruto alisema magaidi 100 waliuawa kwenye operesheni iliyotekelezwa na jeshi punde tu baada ya mauaji ya abiria 28.
Rais Uhuru Kenyatata hata hivyo anakabiliwa na kibarua kigumu wakati huu ambapo visa vya ukosefu wa usalama vinashuhudiwa kila uchao katika sehemu mbali mbali za nchi.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri:Josephat Charo