1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiSomalia

Al-Shabaab wavamia hoteli Mogadishu

28 Novemba 2022

Kundi la kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia limeishambulia hoteli moja karibu na makaazi ya rais katika mji mkuu, Mogadishu, ambako hadi sasa watu wameshauawa na huku mapambano yakiendelea.

Somalia Militants Twitter
Picha: picture alliance / AP Photo

Uvamizi dhidi ya hoteli hiyo iitwayo Villa Rose ulianza Jumapili (Novemba 27), ambapo washambuliaji wa kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida, walitumia bunduki na mabomu kuingia ndani. 

Afisa mmoja wa polisi aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba baadhi ya maafisa wa serikali walilazimika kukimbia kwa kutumia madirisha ya hoteli hiyo.

Mkaazi mmoja, Ismail Haji, anayeishi karibu na hoteli hiyo ameiambia Reuters kwamba kufikia asubuhi ya leo, ikiwa ni zaidi ya masaa 12 tangu uvamizi kuanza, bado kulikuwa na "milio mikubwa ya silaha ndani ya hoteli" na kwamba bado walikuwa wanaendelea kusalia majumbani mwao tangu mzingiro wa vyombo vya usalama uanze usiku wa jana.

Vikosi maalum vya usalama, vifahamikavyo kama Gaashaan na Haramcad, vilichukuwa uratibu wa operesheni hiyo, kwa mujibu wa afisa mmoja wa polisi aliyepo kwenye eneo la tukio. 

Moja ya mashambulizi ya Al-Shabaab mjini Mogadishu.Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/dpa/picture alliance

"Wapiganaji walioanzisha mashambulizi bado wanapambana ndani ya hoteli dhidi ya vikosi vya Haramcad na Gaashaan, na maafisa wa usalama wanajaribu kuwaokowa watu waliokwama ndani ya hoteli," alisema afisa huyo, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Watu wanne wauawa

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, watu waliokwishauawa hadi sasa wamefikia wanne kwenye hoteli hiyo ambayo kawaida hutumiwa na maafisa wa serikali mjini Mogadishu kwa mikutano. 

Afisa mmoja wa usalama wa taifa, Mohamed Dahir, aliiambia AFP kwamba washambuliaji wamejificha kwenye chumba kimoja cha hoteli hiyo huku wakiwa wamezungukwa na vikosi vya serikali.

Hotali iliyoshambuliwa na al-Shabaab mwezi Agosti 2022.Picha: Hassan Ali Elmi/AFP

Kwa mujibu wa afisa huyo, miongoni mwa waliojeruhiwa walikuwa maafisa wa serikali, lakini karibuni watafanikiwa kuidhibiti hali.

Bunge lasitisha vikao

Bunge la Somalia lilisema kuwa lilipaswa kusitisha vikao vya mabaraza yake yote mawili kutokana na mashambulizi hayo. 

Kupitia taarifa iliyotumwa kwenye ukurasa rasmi wa Facebook wa bunge hilo, wajumbe wote wa mabaraza hayo ya bunge waliarifiwa kuahirishwa kwa mkutano uliokuwa umepangwa siku ya Jumatatu (Novemba 28).

Kundi la Al-Shabaab ambalo limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Somalia.Picha: Mariel Müller

Kundi laal-Shabaab, ambalo linataka kuiangusha serikali na kuanzisha utawala unaofuata tafsiri ya siasa kali ya Sharia za Kiislamu, limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara mjini Mogadishu na kwengineko nchini Somalia.

Mnamo tarehe 29 Oktoba, magari mawili yaliyojaa mabomu yaliripuka mjini Mogadishu yakifuatiwa na milio ya risasi, ambapo watu 121 waliuawa na 333 kujeruhiwa.

Hayo yalikuwa mashambulizi mabaya kabisa kufanyika kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Rais Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa mwaka huu, ameanzisha operesheni kali ya kijeshi dhidi ya kundi hilo. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW