1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab yadai mateka 137 wamefariki

25 Septemba 2013

Kundi la Al-Shabaab limedai siku ya Jumatano kuwa mateka 137 waliowachukua wamekufa katika uvamizi wa kituo cha biashara, idadi ambayo ni vigumu kuithibitisha na kubwa kuliko idadi iliyotangazwa kuwa hawajulikani walipo.

Rais Uhuru Kenyatta, akihutubia taifa na kutangaza kumalizika kwa uvamizi wa kundi la Al-Shabaab siku ya Jumanne.
Rais Uhuru Kenyatta, akihutubia taifa na kutangaza kumalizika kwa uvamizi wa kundi la Al-Shabaab siku ya Jumanne.Picha: Reuters

Wapiganaji hao walio na mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, katika ujumbe waliouweka katika mtandao wa kijamii wa twitter, walisema mateka 137 waliokuwa wanashikiliwa na mujahedeen walikufa. Waliwashtumu pia wanajeshi wa Kenya kwa kutumia vifaa vya kemikali kukomesha mkwamo huo uliodumu kwa siku nne. "Katika hatua ya uoga wa dhahiri, vikosi vya Kenya kwa maksudi vilitumia vilipuzi vilivyokuwa na kemikali," ulisema ujumbe mmoja na kuongeza kuwa, "ili kufunika uhalifu wao, serikali ya Kenya iliendesha zoezi la kuliporomosha jengo, na kuuzika ushahidi na mateka wote chini ya vifusi."

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alitangaza kumalizika kwa umwagaji huo wa damu uliodumu kwa saa 80 jioni ya Jumanne, ambao ulisababisha vifo vya raia 61 na maafisa sita wa vikosi vya usalama. Polisi ilisema idadi hiyo ya vifo ingeweza kuongezeka, ambapo shirika la misaada la Msalaba mwekundu liliorodhesha watu 63 ambao bado hawajulikani walipo. Hakukuwa na kauli kutoka serikali ya Kenya kuhusiana na madai hayo, lakini Al-Shabaab wamekuwa wakitoa madai ya ajabu huko nyuma, hasa kupitia akaunti yao kwenye mtandao wa twitter.

Wanajeshi wa ulinzi wa Kenya wakijiandaa kuingia jengo la Westgate kupambana na wavamizi.Picha: Reuters

Kundi hilo lilisema lilifanya shambulizi hilo katika kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kutokana na kujiingiza nchini Somalia kupambana na wanamgambo hao. Katika moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika historia ya Kenya, wapiganaji hao waliingia katika jengo la maduka la Westagate lenye ghorofa nne, ambalo linamilikiwa kwa sehemu na raia wa Israel, mchana wa Jumamosi, na kuanza kuwashambulia wanunuzi kwa risasi na kuripua maguruneti.

Kenya ilianza siku tatu za maombolezi rasmi Jumatano, ambapo bendera za taifa zinapepea nusu mlingoti, huku wafanyakazi wa uokozi wakisafisha mabaki ya jengo la Westgate kutafuta miili ya wahanga wa tukio hilo. Karibu watu 200 walijeruhiwa katika uvamizi huo wa siku nne, ambao ulishuhudia mapambano makali kati ya wapiganaji na vikosi vya usalama vya Kenya katika jengo hilo, ambalo ndicho kituo kikubwa zaidi cha biashara na maarufu kwa watu wenye uwezo nchini Kenya, wanadiplomasia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na watalaamu wengine.

Raia wa Uingereza akamatwa
Wakati huo huo, raia wa Uingereza alikamatwa mjini Nairobi kufuatia shambulio hilo, ofisi ya mambo ya kigeni ilisema Jumanne mjini London. Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Daily Mail, raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 35 mwenye asili ya Somalia, alikamatwa katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta wakati akijaribu kuondoka nchini Kenya kwa ndege ya Uturuki.

Msemaji wa Ofisi ya mambo ya kigeni alikataa kuzungumzia ripoti hiyo, akisema serikali ya Uingereza ilikuwa inafahamu juu ya kukamatwa kwa Muingireza huyo, na ilikuwa tayari kutoa msaada wa kibalozi. Chanzo kutoka idara ya kupambana na ugaidi katika jeshi la polisi la Kenya kililiambia shirika la habari la Reuters kuwa raia wa Uingereza mwenye asili ya Somalia alikamatwa na kuzuiwa katika uwanja wa ndege baada ya kukosa ndege yake, na kwamba alikuwa anahojiwa. Lakini hakikutoa taarifa zaidi.

Moshi ukifuka kutoka jengo la Westgate. Ghorofa tatu za jengo hilo ziliporomoka.Picha: picture-alliance/dpa

Gazeti la Daily Mail lilisema kuwa mwanamume huyo alizua wasiwasi uwanjani kwa sababu alikuwa na jeraha usoni mwake, alikuwa amevaa miwani myeusi, na mwenendo wake ulikuwa unazua mashaka. Gazeti hilo lilisema kuwa hati ya kusafiria ya mwanamume huyo ilionekana kuwa halali na ilikuwa na viza ya Kenya, ingawa hakukuwa na mhuri wa kuonyesha lini na vipi aliingia nchini Kenya.

Uganda yasema vita dhidi ya Al-Shabaab bado vigumu
Mkuu wa majeshi ya Uganda Jenerali Katumba Wamala alisema vikosi vya Umoja wa Afrika vinavyopambana na Al-Shabaab nchini Somalia vinakabiliwa na changamoto za uwezeshwaji, na kwamba vinaweza visimalize operesheni yake katika muda uliopangwa kutokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha, anaripoti mwandishi wa DW mjini Kampala, Leylah Ndinda. Katumba alisema kwa sasa hawawezi kuingia katika maeneo mapya wanakojificha al-Shabaab kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na hata upungufu wa wanajeshi, na kwamba tayari wamekwisha wasiliana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuhusiana na changamoto hizi.

Jenerali Katumba Wamala alisema pamoja na ukweli kwamba kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, AMISOM, kinaweza kuendelea na operesheni zake, inawezekana wakachukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa. Mataifa yanayochangia wanajeshi nchini Somalia, yalisema kuwa yalitaka kuondoka nchini humo ifikapo mwaka 2016. Mkuu huyo wa majeshi ya Uganda, UPDF, sasa anapendekeza kuwa kama Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa hawawezi kuiwezesha AMISOM, basi wajikite katika kutoa mafunzo kwa jeshi la Somalia, na kutumia raslimali zilizopo kuwalipa mishahara.

Mkuu wa jeshi la Uganda, UPDF, Jenerali Katumba Wamala.Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Akizungumzia uvumi kuwa AMISOM inaweza kugeuzwa kuwa kikosi cha Umoja wa Mataifa, Jenerali Wamala alisema kulingana na uzoefu wa huko nyuma, Wasomali wanawaamini sana wanajeshi wa Afrika kuliko wa Umoja wa Mataifa. Uganda ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia, ikitumai kuwadhoofisha wapiganaji wa Al-Shabaab katika kipindi cha muda mfupi.

Polisi Burundi yazingira mitaa ya Waislamu
Naye Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya DW mjini Bujumbura, Amida Issa, anaripoti kuwa polisi ya taifa ya Burundi iliuzingira mtaa wa Buyenzi mjini Bujumbura na Rumonge mkoani Bururi alfajiri ya Jumatano, katika kile ilichosema ni kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabaab na wanaowaunga mkono. Mitaa hiyo yote ina wakaazi wengi ambao ni Waislamu. Burundi ni miongoni mwa mataifa yaliyo na wanajeshi wake nchini Somalia.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre,/ DW Correspondents
Mhariri: Josephat Nyiro Charo