1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabab yauwa wanajeshi 4 wa Uganda

Daniel Gakuba
2 Aprili 2018

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la nchini Somalia wamewauwa wanajeshi wanne wa Uganda katika shambulizi kubwa dhidi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, katika kambi iliyo Kusini mwa Mogadishu.

Somalia Al-Shabaab Kämpfer
Wapiganaji wa kundi la al-Shabab lenye mafungamano na al-QaidaPicha: picture alliance/AP Photo/F. A. Warsameh

 

Shambulizi hilo lilitokea jana Jumapili (Aprili 1) kwenye kambi iliyoko umbali wa kilomita 150 kusini mwa mji mkuu, Mogadishu.

Awali, naibu gavana wa jimbo lilikotokea shambulizi hilo, Ali Noor Mohamed, hakubainisha idadi ya waliouawa, lakini alikiri kuwa wanajeshi kadhaa wa Uganda walipoteza maisha.

Baadaye, msemaji wa jeshi la Uganda, Brigedia Richard Karemire, alithibitisha kuwa al-Shabaab imewauwa wanajeshi  wao wanne na kujeruhi wengine sita. Kundi la al-Shabaab kwa upande wake limedai kuwauwa wanajeshi 59 wa Uganda.

Pia, kundi hilo kupitia kituo chake cha redio cha Andalus limesema wapiganaji wake 14 wameuawa katika shambulizi la jana kwenye kambi ya Buula-Mareer. Msemaji wa jeshi la Uganda amesema idadi ya wanamgambo wa al-Shabab waliouawa ni 30. Umoja wa Afrika haukutoa tamko lolote kuhusu kilichotokea.

''Tumeona vifaru na magari mengine ya kijeshi ya Umoja wa Afrika yakiwa katika barabara nje ya mji wenye kambi iliyoshambuliwa'', alisema Maryam Ali ambaye ameshuhudia shambulizi hilo, na kuongeza kuwa baadaye aliweza kukimbia  yeye na watoto wake sita, kunusuru maisha yao.

Rais Mohamed aapa kuiangamiza al-Shabab

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa SomaliaPicha: DW/Y. G/Egziabhare

Kundi la al-Shabaab, ambalo linapigania kunzisha utawala wa Kiislamu nchini Somalia, mara kwa mara hufanya mashambulizi dhidi ya majengo ya serikali mjini Mogadishu, na pia hoteli na migahawa katika nchi hiyo ya Upembe wa Afrika inayokabiliwa na mzozo wa muda mrefu. Mwezi Oktoba, shambulizi baya zaidi liliuwa watu zaidi ya 500 mjini Mogadishu.

Tangu kutokea shambulizi hilo, Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed ameapa kuliangamiza kundi la al-Shabab, akiungwa mkono na umma, ambao umeingia kwa maelfu mitaani, katika maandamano ya kutaka kundi hilo lipigwe vita hadi kushindwa. Hata hivyo, kundi hilo ambalo lilifukuzwa mjini Mogadishu mwaka 2011, bado linashikilia maeneo makubwa ya vijijini.

Mwezi uliopita, nchi za Mashariki mwa Afrika zinazochangia wanajeshi 22,000 katika ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kulinda amani nchini Somalia, AMISOM, wameutaka Umoja wa Mataifa kutafakari upya azma yake ya kuuhitimisha ujumbe huo ifikapo mwaka 2020, wakisema hatua hiyo inaweza kuhujumu hatua iliyopigwa katika kuleta utulivu nchini Somalia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW