1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Sisi aahidi kuliunga mkono jeshi la Sudan

5 Novemba 2024

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ameahidi kuendelea kuliunga mkono jeshi nchini Sudan wakati wa mkutano na mkuu wa jeshi hilo. Haya ni kulingana na taarifa iliyotolewa na afisi ya al-Sisi.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-SisiPicha: John Macdougall/AP Photo/picture alliance

 Wakati wa mazungumzo hayo na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Sisi pia ametoa wito wa usitishwaji wa mapigano na umwagikaji damu.

Burhan kwa upande wake amezisifu juhudi za dhati za Misri za kutaka kusitisha mapigano nchini Sudan.

Soma pia:Mkuu wa jeshi Sudan kukutana na rais wa Misri leo

Burhan na Sisi kwa muda mrefu wameonekana kama marafiki na kundi la wanamgambo la RSF mwezi uliopita liliituhumu Misri kwa kuwashambulia wanamgambo wake kwa makombora ya angani, madai yaliyokanushwa na Misri.

Jeshi la Sudan pamoja na RSF wote wamehusishwa na kufanya unyama katika vita hivyo ikiwemo kuwalenga raia, kuyashambulia maeneo ya makaazi na kufanya uporaji na kuzuia misaada.