1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Al-Zawahri ni nani na kwa nini ameuawa na Marekani?

Sylvia Mwehozi
2 Agosti 2022

Shambulio la Marekani la ndege isiyo na rubani nchini Afghanistan ndilo limemuua kiongozi wa Al-Qaeda Ayman al-Zawahri ambaye alimsaidia Osama bin Laden kupanga mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Al Kaida Anführer Aiman az Zawahiri
Picha: Mazhar Ali Khan/AP Photo/picture alliance

Taarifa za kifo cha Ayman al-Zawahri zilitolewa na rais Joe Biden siku ya Jumatatu, ikiwa ni miezi 11 tangu vikosi vya Marekani vilipofungasha virago na kuondoka Afghanistan. Mauaji ya kiongozi hayo yanachukuliwa kama hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugaidi. Lakini je al-Zawahri ni nani na kwa nini alikuwa akisakwa kwa muda mrefu na Marekani?

Wamarekani walioishi kupita mashambulizi ya Septemba 11 wanaweza wasikumbuke jina la al-Zawahri, lakini wengi wao wanafahamu sura yake kwa zaidi ya miongo miwili. Kwanza, mwanaume aliyevalia miwani, akitabasamu kidogo, akionyeshwa picha yake mara kwa mara kando ya Osama bin Laden wakati wawili hao walipokuwa wakipanga mashambulizi dhidi ya Marekani.

Al-Zawahri alizaliwa nchini Misri mwaka 1951 katika kitongoji kimoja mjini Cairo. Amekuwa na misimamo ya kidini tangu ujana wake, akijitumbukiza katika tawi la Uislamu wa Kisuni uliotaka kuchukua nafasi ya serikali ya Misri na nyinginezo katika mataifa ya kiarabu kwa kuzingatia misimamo mikali ya utawala wa Kiislamu.

Osama bin Laden (kulia) akimsikiliza Ayman al-ZawahriPicha: Al-Jazeera/APTN/picture alliance

Al-Zawahri alifanya kazi kama daktari wa upasuaji macho wakati akiwa kijana, lakini akizunguka katika maeneo ya Asia ya Kati na Mashariki ya Kati, akishuhudia vita vya Afghanistan dhidi ya wavamizi wa Kisovieti. Alikutana na Osama bin Laden wakati akiwa kijana na wapiganaji wengine wa kiarabu ambao walikuwa na lengo la kuvifurusha vikosi vya Kisovieti.

Alikuwa miongoni mwa mamia ya wapiganaji waliokamatwa na kuteswa katika magereza ya Misri baada ya mauaji ya rais Anwar Sadat mwaka 1981. Wajuzi wanasema uzoefu huo ulimfanya kuwa na misimamo mikali zaidi. Miaka saba baadaye, Al-Zawahri alikuwa sambamba na bin Laden wakati alipoanzisha kundi la al-qaeda. Al-Zawahri aliunganisha kundi lake la wanamgambo wa Misri na kundi la al-Qaida.

Kwanini Al-Zawahri alikuwa na umuhimu kwa Al-qaeda?

Je kuuawa kwa kiongozi wa al-Qaeda ndiyo mwisho wa ugaidi?

This browser does not support the audio element.

Baada ya miaka kadhaa ya kukusanya kimya kimya washambuliaji wa kujitoa mhanga, fedha na mipango ya shambulio la Septemba 11, al Zawahri alihakikisha kwamba ananusurika na msako wa kimataifa. Akiwa mafichoni baada ya mashambulizi ya Septemba 11, al Zawahri aliujenga upya uongozi wa Al-Qaeda katika mkoa unaopakana na Afghanistan na Pakistan na alikuwa kiongozi mkuu katika matawi ya Iraq, Asia, Yemen na kwingineko.

Baada ya Septemba 11, 2001 kundi hilo lilifanya mashambulizi kadhaa yasiyokoma. Huko Bali, Mombasa, Riyadh, Jakarta, Istanbul, London na kwingineko. Mashambulizi yaliyowaua watu 52 huko London mwaka 2005 yalikuwa ni miongoni mwa mashambulizi ya kusikitisha dhidi ya nchi za magharibi. Marekani na washirika zake walianzisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, mashambulizi ya kushutukiza na makombora na kuwaua wapiganaji walio na mafungamano na Al-qaeda na kuvunja mtandao.

Vipi alinaswa na Marekani?

Ayman al-ZawahriPicha: Militant video via SITE/AP Photo/picture alliance

Wakati jua lilipochomoza siku ya Jumapili, al Zawahri alitoka nje kwenye roshani ya makaazi yake mjini Kabul. Rada za Marekani tayari zilikwisha fahamu kuwa kuna mtu hutoka nje mara kwa mara na pengine ndiye yeye. Siku hiyo ndege isiyo na rubani ya Marekani ilirusha kombora dhidi ya kiongozi huyo aliyekuwa amesimama nje na kumuua.

Wachambuzi wanaamini uwepo wake nchini Afghanistan ulikuwa unashukiwa sana na baadhi ya watu. Intelijensia za Marekani zilifahamu kwamba mke wake pamoja na ndugu wengine wa familia walihamia katika nyumba ya usalama mjini Kabul hivi karibuni. Kiongozi huyo aliwafuata ndugu zake baadae. Maafisa wa Marekani, viongozi wakuu wa ulimwengu na Biden, kwa miezi kadhaa wamekuwa wakithibitisha kwa uangalifu juu ya uhakika wa utambulisho wake na kitendo cha mtu anayetoka barazani mara kwa mara akiwa peke yake ikiwa ndiye na hapo ndipo walipanga shambulio.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW