Alaba na Davis kuikosa mechi dhidi ya Freiburg
19 Juni 2020Wakati mabingwa wapya wa ligi kuu ya soka ya Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich wakitarajia kuteremka dimbani Jumamosi tarehe (20.06.2020), kukabiliana uso kwa uso na timu ya soka ya Freiburg, kocha wa wababe hao kutoka jimbo la Bavaria atafanya mabadiliko katika kikosi chake cha kwanza huku wakiwa tayari wamekwishalitwaa taji la Bundesliga msimu huu.
Beki wa kushoto Alphonso Davies amesimamishwa wakati mchezaji hodari beki wa kati David Alaba hatakuwepo kutokana na kuwa majeruhi katika kifundo cha mguu wake.
"David atakosa katika mchezo huo," kocha Hansi Flick, aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa (19.06.2020). Serge Gnabry hatakuwepo katika mchezo huo kutokana na maumivu ya mgongo naye Ivan Perisic akipata dhoruba katika mechi iliyopita.
"Tutafanya mabadiliko mawili au moja," alisema Flick. Javi Martinez anaweza kuchukua nafasi ya Alaba kama mlinzi wa kati. Bingwa wa dunia raia wa Ufaransa, Lucas Hernandez, anaweza kuchukua nafasi ya Davies kwa upande wa kushoto.
Bayern imedhamiria kutokuwa mteremko katika michezo yake iliyosalia baada ya kushinda taji la Bundesliga msimu huu na Julai 4 mechi ya fainali ya kombe la shirikisho DFB Pokal dhidi ya Bayer Leverkusen na mechi za ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
"Sio kwamba tuna ubingwa na ndio maana tumefanya hivyo," alisema Flick. Ni muhimu kuendeleza moto wa ushindi. Tunataka kumaliza michezo yote miwili ya ligi kwa mafanikio.
dpa