1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aleppo yaangukia mikononi mwa Assad

14 Desemba 2016

Usitishaji mapigano bado unaendelea mjini Aleppo baada ya kuangukia rasmi mikononi mwa serikali, lakini uhamishwaji wa raia na waasi umesita, huku kukiwa na taarifa za vikosi vya serikali na kuwauwa raia.

Syrien Familie mit verletztem Kind in Aleppo
Picha: Reuters/A. Ismail

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, amesema hivi leo kuwa mkanyanyiko unaoshuhudiwa sasa mashariki mwa Aleppo katika kuwahamisha raia na wapiganaji wa waasi unadhihirisha namna ilivyo muhimu kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kulisimamia zoezi hilo.

"Ufaransa inataka waangalizi wa Umoja wa Mataifa wawepo na mashirika ya misaada kama vile Msalaba Mwekundu lazima yaingilie kati," alisema Ayrault.

Kwa mujibu wa makubaliano ya awali, uhamishwaji huo ulikuwa uanze alfajiri ya leo (Novemba 14), lakini hadi sasa hakuna aliyehamishwa na huenda ukaanza kesho.

Upinzani unasema kuwa wanajeshi wa Iran na wanamgambo wa Kishia wanaomuunga mkono Rais Bashar al-Assad wanahusika na ucheleweshwaji huo.

"Kilichozuwia kutekelezwa makubaliano kwa sasa ni khiyana ya Iran tu, lakini makubaliano bado yapo, usitishaji mapigano unaendelea hadi sasa," alisema kamanda mmoja wa kundi la Nour al-Din al-Zinki akiwa mashariki mwa Aleppo.

Mchango wa Urusi na Uturuki

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, ambayo yalifikiwa kwa msaada wa Urusi inayomuunga mkono Assad na Uturuki inayowaunga mkono waasi, umehitimisha mapigano ya miaka mitano kwenye mji huo na huku yakimpa Assad ushindi mkubwa baada ya miaka yote hiyo ya vita.

Kikosi cha jeshi la Syria kikiingia mashariki mwa Aleppo huku mji huo ukianguka kutoka mikono ya waasi baada ya miaka mitano ya mapigano.Picha: Reuters/O Sanadiki

Mapema leo, Umoja wa Mataifa ulisema hauhusiki na mipango ya kuwahamisha wapiganaji na raia kutoka mashariki mwa Aleppo, lakini uko tayari kusaidia.

"Umoja wa Mataifa uko tayari kuwezesha uondokaji wa hiyari na salama wa majeruhi, wagonjwa na raia walio hatarini kwenye maeno yaliyozingirwa na mji huo." Ilisema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Huduma za Kibinaadamu ya Umoja huo (OCHA).

Hayo yakiendelea, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, kulikuwa na majibizano makali ya maneno kati ya Marekani na Urusi na Syria kuhusiana na shutuma za vikosi vya serikali kupita nyumba kwa nyumba na kuwapiga risasi raia wasiokuwa na hatia.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Rupert Colville, amesema wamepokea taarifa za watu kupigwa risasi mitaani wakati wanapojaribu kukimbia, huku 82 wakiuawa ndani ya majumba yao. 

Jeshi la Syria limekanusha kuwauwa au kuwatesa waasi liliowakamata, huku Urusi ikisema waliwashikilia zaidi ya watu 100,000 kama ngao mashariki mwa Aleppo.

Hali ya wasiwasi imetanda miongoni mwa waliosalia kwenye eneo hilo.

Picha zinazotumwa na wanaharakati walio huko zinaonesha watu wakichupa maiti waliotapakaa mitaani kukimbilia maeneo yaliyo mikononi mwa serikali, huku wengine wakisalia majumbani: "Tunangojea mauti yatufike, na sasa hamuwezi tena kutusaidia," mmoja wao alisema kwa njia ya Skype.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo