1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Alexei Navalny afariki akiwa gerezani

16 Februari 2024

Mwanasiasa mkuu wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny, ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa Rais Vladimir Putin amefariki dunia siku ya Ijumaa katika gereza la Arctic ambako alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 19.

Urusi I Picha ya Alexei Navalny ikiwa imewekewa shada la maua
Shada la maua likiwa limewekwa kwenye picha ya Mpinzani mkuu wa serikali ya Urusi Alexei NavalnyPicha: Gonzalo Fuentes/REUTERS

Vyombo vya habari vya Urusi vinadai kuwa madaktari walijaribu kuyaokoa maisha ya Navalny bila mafanikio, lakini viongozi mbalimbali duniani wamelaani kuhusu kifo hicho na kuitupia lawama serikali ya Putin.

Mamlaka ya magereza ya shirikisho la Urusi imesema Alexei Navalny mwenye umri wa miaka 47 na ambaye aliwahi kulengwa na kitendo cha kuwekewa sumu kabla ya kwenda jela, alipata hitilafu ya kiafya mara baada ya matembezi kidogo katika jela hiyo, na kwamba hali yake ilibadilika ghafla na kupoteza fahamu.     

Wameendelea kuwa wahudumu wa afya walianza mara moja kutoa matibabu kwa Navalny na kwamba kwa zaidi ya nusu saa walijaribu kuokoa maisha ya mwanaharakati huyo ambaye pia alikuwa mkuu wa Shirika la Kupambana na Ufisadi nchini Urusi.

Mke wa mpinzani wa Urusi Alexei Navalny, Bi Yulia Navalnaya akihutubia mkutano wa usalama mjini Munich Ujerumani: 16.02.2024Picha: THOMAS KIENZLE/AFP/Getty Images

Hatimaye, wahudumu wa afya walithibitisha  kifo Navalny  ingawa hadi sasa sababu za kifo chake hazijawekwa wazi. Kamati ya Uchunguzi ya Urusi imesema imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo hicho.

Soma pia: Mpinzani wa Putin Navalny ahamishiwa gereza Aktiki

Mawakili wa Navalny umesema haujafahamishwa kuhusu kifo hicho lakini wakili wake alikuwa akielekea katika gereza la mbali la Kharp katika eneo la Arctic ili kupata taarifa zaidi.

Katika mitaa ya Moscow, raia wa Urusi hasa vijana wameshtushwa na taarifa hii huku wakijawa na hofu kuhusu mustakabali wa wapinzani katika taifa hilo.

Mama wa Navalny Bi Lyudmila Navalnaya, amenukuliwa na vyombo vya habari vya Urusi akisema hataki kusikia salamu za rambirambi, maana anasema walionana na Navalny gerezani mnamo Februari 12 akiwa hai, mwenye afya njema na mwenye furaha. Mke wa Navalny amesema Putin ni lazima aadhibiwe kwa 'unyama' wote  alioufanya dhidi ya mumewe.

Viongozi wa Magharibi wainyooshea kidole Urusi

Rais wa Urusi Vladimir Putin amenyooshewa kidole na kutajwa kuwa anahusika moja kwa moja.  Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amesema kuwa Urusi inahusika moja kwa moja na  kifo cha Navalny:

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris akihutubia mkutano wa usalama wa mjini Munich nchini Ujerumani: 16.02.2024Picha: Johannes Simon/Getty Images

" Tumepokea taarifa kwamba Alexei Navalny amefariki dunia nchini Urusi. Hakika hii ni habari mbaya na ambayo tunajaribu kuithibitisha. Maombi yangu yawe pamoja na familia yake, akiwemo mke wake, Yulia ambaye yuko nasi leo. Na ikiwa itathibitishwa, hii itakuwa ishara zaidi ya ukatili wa Putin. Licha ya yote wanayosema, tuwe wawazi, Urusi inawajibika na tutazungumza zaidi juu ya hili hapo baadaye."

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron amesema Vladimir Putin anapaswa kuwajibishwa na kifo hicho.

Soma pia: Kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny ahukumiwa miaka mingine 19 jela

Aidha, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amedhihirsha wasiwasi wake kuhusu taarifa za kifo cha Alexei Navalny na kusema kuwa hilo lazima liwe kama onyo kwa ulimwengu mzima.

Viongozi wengina kama Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte wakisisitiza kwamba kifo hiki cha Navalny kinadhihirisha wazi utawala wa kikatili na kidhalimu wa serikali ya Vladimir Putin.

(Vyanzo: ap, afp,rtre,dpa)