1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria yamrudisha nyumbani balozi wake kutoka Ufaransa

Zainab Aziz Mhariri: John Juma
3 Oktoba 2021

Algeria imemwita nyumbani balozi wake wa Ufaransa kwa mashauriano baada ya kile ilichokiita "Maoni potofu" yalitolewa na Rais wa Ufaransa Emmanueln Macron.

Flaggen | Frankreich & Algerien
Picha: Valery Hache/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa tamko la ofisi ya rais wa Algeria lilotolewa Jumamosi, Algeria imeelezea kukataa kwake kuingiliwa katika mambo yake ya ndani. Kutokana na hali hiyo isiyokubalika, Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amesema aliamua kumrudisha nyumbani mara moja balozi wake wa Ufaransa.

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune Picha: Billal Bensalem/NurPhoto/imago images

Jarida la kila siku la Ufaransa, Le Monde liliripoti kwamba Macron alitoa maoni yasiyopendeza juu ya Algeria, koloni lake la zamani wakati wa mkutano mnamo siku ya Alhamisi alipokuta na wazawa wa Waalgeria waliopigana kwenye vita vya uhuru.

Macron alisema nini?

Inasemekana Macron alisema nchi hiyo inatawaliwa na mfumo wa kisiasa ulio chini ya jeshi na alielezea kuwa historia ya Algeria imeandikwa upya kabisa na kwamba haina ukweli isipokuwa inaegemea chuki dhidi ya Ufaransa. Matamshi hayo ya Macron yalinukuliwa sana na vyombo vya habari vya Algeria.

Sera ya uhamiaji ya Ufaransa ikoje?

Mapema wiki hii, serikali ya Algeria ilisema ilimwita balozi wa Ufaransa mjini Algiers kujibu juu ya kupunguzwa idadi ya viza kwa raia wa Algeria wanaotaka kwenda Ufaransa.

Msemaji wa serikali ya Ufaransa Gabriel Attal aliiambia redio ya Europe 1 mnamo siku ya Jumanne kwamba Ufaransa itapunguza nusu ya idadi ya viza zinazotolewa kwa raia kutoka Algeria na Moroko,Tunisia kwa karibu theluthi moja.

Ufaransa ilisema uamuzi huo ni kujibu serikali za Maghreb zinazokataa kuwachukua wahamiaji haramu walioamriwa kurudi nyumbani na Ufaransa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AFP

Malalamiko

Wizara ya Mambo ya nje ya Algeria imeelezea hatua hiyo kama uamuzi wa upande mmoja wa serikali ya Ufaransa na kukiita kitendo hicho kuwa ni kibaya na ambacho kimesababisha mkanganyiko na utata juu ya nini hasa nia na lengo lake. Wizara ya mambo ya nje ya Algeria ilikabidhi pingamizi rasmi kwa balozi wa Ufaransa Francois Gouyette.

Hatua hiyo ya Jumamosi ni ya mara ya pili ambapo Algeria ilimwita kurejea nyumbani balozi wake kutoka Ufaransa. Mnamo Mei 2020, nchi hiyo ilimrudisha balozi wake baada ya vyombo vya habari vya Ufaransa kutangaza waraka kuhusu harakati za maandamano yaliyoandaliwa na vuguvugu la Hirak la Algeria linalopigania demokrasia.

Vyanzo://RTRE/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW