1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ALGIERS : Polisario yaonya juu ya vita vya Sahara ya Magharibi

22 Mei 2005

Kiongozi wa Polisario chama kinachopigania uhuru wa Sahara ya Magharibi inayoshikiliwa na Morocco ameonya hapo jana kuanza tena vita ambavyo vimemalizika kwa usitishaji wa mapigano hapo mwaka 1991.

Mohamed Abdelaziz amesema katika sherehe za kuadhimisha miaka 32 ya kuundwa kwa Polisario kwamba wananchi wa Sahrawi hawawezi kuendelea kukunja mikono yao milele na kwamba watapambana kujipatia haki zao za taifa kwa njia zote za halali ikiwa ni pamoja na kuanza tena mapambano ya silaha.

Morooco iliitwaa Sahara ya Magharibi baada ya mkoloni wake wa zamani Uhispania kujitowa kwenye eneo hilo kubwa la jangwa lenye utajiri wa madini ya phosphate hapo mwaka 1975 na Polisario ikachukuwa silaha mwaka uliofuatia kupigania uhuru wao.

Aziz ameisihi serikali ya Morocco kusikiliza sauti ya busara na kutii sheria ya kimataifa kwa kusema kwamba hatua ya Morocco kukataa pendekezo linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuitisha kura ya maoni juu ya wananchi wa Sahara ya Magharibi kujiamulia mambo yao wenyewe ni ya hatari.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamewekwa kwenye eneo hilo tokea usitishaji wa mapigano wa mwaka 1991 lakini jitihada za kimataifa kuutatuwa mzozo huo kati ya pande hizo mbili zimeshindwa.

Mfalme Mohamed wa Morroco hapo mwezi wa Januari amesema nchi yake katu haitoiachilia Sahara ya Magharibi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW