Ali Larijani: Mtu mwenye ushawishi mkubwa usiyo rasmi Iran
17 Machi 2026
Shambulizi la anga lililolenga makazi ya Ayatollah Ali Khamenei mjini Tehran — moja ya mashambulizi ya mwanzo katika vita vya sasa kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran — lilimuua kiongozi huyo mkuu mwenye umri wa miaka 86 pamoja na sehemu kubwa ya muundo wa uongozi wa kijeshi wa Iran.
Iran bado haijaamua nani atakuwa kiongozi ajaye. Hata hivyo, kwa sasa pengo la madaraka linaonekana kujazwa na afisa mkuu wa usalama wa taifa Ali Larijani, anayeripotiwa kuwa mmoja wa watu wachache waliokuwa wakiaminiwa na Khamenei kuhakikisha utawala unaendelea iwapo angefariki.
Takribani saa 24 baada ya shambulizi la Tehran, Larijani alijitokeza kwenye televisheni ya taifa na mitandao ya kijamii kuishutumu Marekani na Israel kwa "kuwasha moto katika moyo wa taifa la Iran.” Alisema: "Tutachoma mioyo yao. Tutawafanya wahalifu wa Kizayuni na Wamarekani wasio na haya wajutie vitendo vyao.”
Ingawa kauli kali kama hizo si za kushangaza kwa Larijani, pia amejijengea sifa ya kimataifa kama mwanasiasa mwenye msimamo wa vitendo. Katika miongo kadhaa ya kazi yake ya kisiasa, amejidhihirisha kuwa mpatanishi mwenye uwezo katika mazungumzo na Urusi, China na hata Marekani, pamoja na kuwa mpangaji wa nguvu ndani ya utawala wa Iran.
Hata hivyo, huku Marekani na Iran zikiwa katika vita vya wazi, Larijani mwenye umri wa miaka 67 amekataa madai ya Rais Donald Trump kwamba viongozi wa Iran wanataka mazungumzo. "Hatutaingia mazungumzo na Marekani,” alijibu kupitia mtandao wa X.
Nafasi mpya ya Larijani juu ya uongozi wa Iran ni ya kushangaza kwa kuwa hana uwezekano wa kurithi rasmi nafasi ya Khamenei. Wote Khamenei na mtangulizi wake Ruhollah Khomeini walikuwa wanazuoni wakuu wa dini ya Kiislamu ya Kishia walioteuliwa kuwa viongozi wakuu wa dola ya kidini iliyoanzishwa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.
Kina Kennedy Wa Iran
Larijani, aliyezaliwa Iraq, si mwanazuoni wa dini, lakini anatoka katika familia yenye uhusiano mkubwa wa kidini na kisiasa ndani ya utawala wa Iran, iliyowahi kuelezwa na jarida la Time kama "Kennedy wa Iran.” Baba yake alikuwa ayatollah mkuu, huku kaka yake Sadeq Larijani pia akiwa ayatollah na aliwahi kuongoza idara ya mahakama ya Iran kati ya 2009 na 2019. Kaka mwingine, Mohammad-Javad Larijani, ni mwanasiasa mwandamizi wa sera za kigeni na mshauri wa marehemu Khamenei. Kabla ya kifo cha ayatollah huyo, kulikuwa na tetesi kwamba familia ya Larijani ilikuwa ikijaribu kumpandisha mmoja wao kuwa kiongozi mkuu ajaye.
Mkwe wake Larijani, marehemu Morteza Motahhari, alikuwa rafiki wa karibu wa Ruhollah Khomeini na msaidizi wake wakati wa mapinduzi ya mwaka 1979.
Hata hivyo, Larijani alijijengea mamlaka kupitia mfumo wa kisiasa wa Iran. Alizaliwa mwaka 1958, alijiunga na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1981 na kuhudumu kama kamanda katika miaka ya mwanzo ya vita vya Iran na Iraq. Alisoma katika chuo cha dini kabla ya kupata shahada ya sayansi ya kompyuta na hisabati, kisha shahada ya uzamili na udaktari katika falsafa ya Magharibi kutoka Chuo Kikuu cha Tehran. Utafiti wake wa kitaaluma ulijikita kwa mwanafalsafa wa Kijerumani Immanuel Kant.
Asukumwa nje na Ahmadinejadi
Akiendelea na masomo yake ya falsafa, alitumia pia historia yake ya kijeshi na uhusiano wa kifamilia kujenga kazi ya kisiasa, akawa waziri wa utamaduni akiwa katika umri wa miaka ya thelathini. Mwaka 1994, Khamenei alimchagua kuwa mkuu wa shirika la utangazaji la taifa, ambapo alikaa kwa muongo mmoja na kulitumia kama chombo cha propaganda ya serikali.
Larijani aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2005 lakini alipata chini ya asilimia sita ya kura katika duru ya kwanza, huku mwanasiasa mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmadinejad akiibuka mshindi.
Baadaye aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa na mpatanishi mkuu wa nyuklia wa Iran, lakini alijiuzulu mwaka 2007 kutokana na tofauti na Ahmadinejad. Migongano na wahafidhina wenye msimamo mkali iliendelea kuathiri kazi yake ya kisiasa, ingawa mwaka 2008 alichaguliwa kuwa spika wa bunge na kushikilia wadhifa huo kwa miaka 12.
Akiwa bungeni, alichangia kupitishwa kwa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani, yaliyolenga kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran badala ya kuondolewa kwa vikwazo. Makubaliano hayo yalifutwa na Trump mwaka 2018.
Larijani azuiwa kushiriki uchaguzi wa 2021 na 2024
Mwaka 2020, Larijani alisimamia makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati wa miaka 25 kati ya Iran na China. Akiwa na nguvu mpya baada ya makubaliano hayo, alijaribu kugombea urais tena mwaka 2021 lakini alizuiwa na Baraza la Walinzi bila sababu rasmi kutolewa. Baadhi walidai aliondolewa kwa sababu binti yake anaishi Marekani na ana pasipoti ya Uingereza, huku wengine wakisema ilifanyika ili kumpa nafasi mgombea aliyependelewa na utawala, Ebrahim Raisi.
Raisi alichaguliwa kuwa rais lakini alifariki katika ajali ya helikopta mwaka 2024. Larijani alijaribu tena kugombea urais lakini alizuiwa tena, huku ushindi ukitwaliwa na mwanasiasa wa wastani Masoud Pezeshkian.
Mwaka jana majira ya joto, Pezeshkian alimrudisha Larijani kuwa mkuu wa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa, na kumfanya kuwa afisa mkuu wa usalama wa Iran kufuatia vita vya siku 12 na Israel. Tangu wakati huo, mamlaka yake na ukaribu wake na Khamenei vimeonekana kumzidi hata rais mwenyewe.
Larijani alionekana kuwa nguvu ya nyuma ya mazungumzo mapya ya nyuklia kati ya Iran na Marekani, na alisafiri mara kadhaa kwenda Moscow kama mjumbe wa Khamenei kwa Rais Vladimir Putin.
Akizungumza na Al Jazeera siku chache kabla ya mashambulizi ya Marekani na Israel, Larijani alisema Iran ilitumia miezi ya karibuni "kujiandaa” kwa vita. "Hatutafuti vita, na hatutaanzisha vita. Lakini wakitulazimisha, tutajibu,” alisema.