Alix Didier aapishwa Waziri Mkuu mpya wa Haiti
12 Novemba 2024Fills-Aime anachukua nafasi ya Garry Conille, aliyeteuliwa mwishoni mwa mwezi Mei, lakini katika siku za karibuni amekabiliwa na shinikizo kubwa la kiuongozi kutoka kwa Baraza la Mpito kuhusiana na uteuzi wa mawaziri.
Amesema, anatambua hali mbaya ambayo Haiti inapitia kwa sasa, lakini ameahidi kuweka nguvu zake zote, uwezo na uzalendo katika kulihudumia taifa hilo lililoathirika vibaya na machafuko.
Kiongozi huyo pamoja na baraza hilo la mpito wanakabiliwa na kitisho kinachotokana na ongezeko la machafuko ya magenge ya wahalifu na wana jukumu kubwa la kuandaa njia ya uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Connile ahoji mamlaka ya baraza ya kumuondoa
Waziri Mkuu anayeondoka Conille kwa upande wake amehoji mamlaka ya baraza hilo ya kumfukuza, hali inayoongeza wasiwasi wa mzozo zaidi wa kisiasa nchini Haiti, taifa ambalo halijafanikiwa kupata rais tangu kuawawa kwa rais Jovenel Moise, mwaka 2021.
Lakini pia hakuna vikao vya bunge, na uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2016.
Taifa hilo kwa muda mrefu limekumbwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, umaskini uliokithiri, majanga ya asili na ghasia za magenge.
Magenge ya Haiti yaendeleza ghasia nje ya mji mkuu
Lakini hali ilizidi kuwa mbaya mwishoni mwa mwezi Februari wakati makundi yenye silaha yalipoanzisha mashambulizi katika mji mkuu Port-au-Prince, yakisema yalitaka kumpindua waziri mkuu wa wakati huo Ariel Henry.
UN yaendelea kutoa wito wa mazungumzo ili kurejesha amani
Henry ambaye hakuchaguliwa na kiongozi ambaye hakupendwa na wengi, aliachia ngazi katikati ya mzozo mkali na kuliachia mamlaka baraza la mpito, linaloungwa mkono kikanda na Marekani.
Alipozungumzia machafuko ya hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizitaka pande zote nchini Haiti "kufanya kazi kwa pamoja" ili kuhakikisha uadilifu katika kipindi cha mpito, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wake Stephane Dujarric siku ya Jumatatu.
Katika miaka ya karibuni magenge ya uhalifu yamedhibiti karibu asilimia 80 ya mji mkuu Port-au-Prince.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema magenge hayo yalikuwa yakichimba mitaro, kutumia ndege zisizo na rubani na kuhifadhi silaha huku wakibadilisha mbinu za kukabiliana na jeshi la polisi linaloongozwa na Kenya.