1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zammel ahukumiwa kifungo cha miaka 35 jela

12 Novemba 2024

Aliyekuwa mgombea urais nchini Tunisia, Ayachi Zammel, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili na miezi minane jela, na kuongeza muda wake jela kufikia miaka 35 kufuatia kesi za awali.

Tunisia
Aliyekuwa mgombea urais Tunisia ahukumiwa kifungo cha miaka 35 jelaPicha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Zammel, mmoja wa wagombea wawili pekee walioruhusiwa kushindana na Rais Kais Saied mwezi uliopita, alikamatwa mapema mwezi Septemba, siku ambayo mamlaka ya uchaguzi iliidhinisha kugombea kwake.

Wakili wake,  Abdessatar Messaoudi, alisema mahakama ya Marouba, karibu na mji mkuu wa Tunis, imetoa hukumu hiyo baada ya kumkuta na hatia ya kughushi ridhaa za kugombea katika uchaguzi huo. Kulingana na wakili wake, Zammel, mwenye umri wa miaka 47, alikuwa akishitakiwa katika kesi 37 tofauti.

Zammel, mbunge wa zamani, mfanyabiashara na mkuu wa chama kidogo cha kiliberali, alipata karibu asilimia saba ya kura za urais, ambapo Saied alishinda zaidi ya asilimia 90, kulingana na tume ya uchaguzi ya Tunisia, ISIE.