1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Bashar al-Assad na familia yake wapewa hifadhi Urusi

9 Desemba 2024

Aliyekuwa rais wa Syria Bashar al-Assad yuko Moscow na familia yake baada ya Urusi kuwapa hifadhi kutokana na sababu za kibinadamu.

Aliyekuwa rais wa Syria Bashar al-Assad
Aliyekuwa rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: Alexei Nikolsky/Sputnik/Kremlin Pool/AP Photo/picture alliance

Hayo yameelezwa Jumapili usiku na Ikulu ya Kremlin, iliyosisitiza kuwa makubaliano yamefikiwa ili kuhakikisha usalama wa kambi za kijeshi za Urusi nchini Syria. Awali Moscow ilisema kambi hizo ziko katika tahadhari kubwa lakini hakukuwa na kitisho dhidi yao kwa sasa.

Assad ameikimbia nchi baada ya waasi kuchukua udhibiti wa mji mkuu Damascus huku akitoa maagizo kwamba ukabidhi wa madaraka ufanyike kwa amani. 

Rais wa Marekani Joe Biden amesema ni lazima Assad awajibishwe kwa vitendo vya mauaji na mateso kwa mamia ya maelfu ya Wasyria. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya hivi leo mkutano wa dharura na wa faragha ili kuijadili hali inayoendelea nchini Syria.

Waasi wa Syria watangaza marufuku ya kutembea usiku

Raia wa Syria mjini Berlin wakisherehekea kuanguka kwa utawala wa AssadPicha: Julius Christian Schreiner/dpa/picture alliance

Waasi wa Syria wametangaza marufuku ya watu kutembea nje usiku hadi saa kumi na moja asubuhi. Tangazo hilo limejiri baada ya waasi hao kuchukua udhibiti wa mji mkuu Damascus na kuuangusha utawala wa Bashar al Assad. Tangazo hilo limejiri baada ya waasi hao kuchukua udhibiti wa mji mkuu Damascus na kuuangusha utawala wa Bashar al Assad.

Waasi hao pia walitangaza kwamba rais Assad ameikimbia nchi na kwamba watakabidhi mamlaka kwa Baraza la mpito. Raia wa Syria wameonekana wakimiminika barabarani, wakishangilia baada ya waasi kusitisha utawala wa kiimla wa familia ya Assad wa miaka 50. 

Raia hao walikusanyika mjini humo wakipeperusha bendera ya taifa hilo. Wengine walionekana wakiingia katika ikulu ya rais  na maeneo mengine ya familia ya Assad baada ya rais na maafisa wengine wa serikali kuikimbia nchi. 

Imeripotiwa pia kwamba watu waliingia katika ubalozi wa Iran mjini Damascus na wakaharibu ofisi za ubalozi huo kando na kupora mali. Kukamilika kwa utawala wa Assad ni pigo kwa Iran na washirika wake ambao wako katika mgogoro wa takriban mwaka mmoja na Israel. 

Kauli ya awali ya Urusi kuhusu kuondoka kwa Assad 

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Syria aliyeondolewa madarakani Bashar Al AssadPicha: SANA/AFP

Awali mshirika wa karibu wa Assad, Urusi, kupitia wizara yake ya kigeni ilisema rais wa Syria Bashar al Assad ameondoka madarakani na kuitoroka nchi huku akitoa maagizo ya ukabidhi wa madaraka kufanyika kwa amani. Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisisitiza kuwa Urusi haikuhusika na mazungumzo ya kuondoka kwake. 

Moscow ilikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya matukio ya Syria na kuhimiza pande zote kujizuwia na vurugu na kusuluhisha masuala yote ya uongozi kupitia njia za kisiasa. Urusi imesema inawasiliana na makundi yote ya upinzani Syria kuhakikisha hilo linafanyika. 

Urusi pia imesema kambi zake za kijeshi ziko katika tahadhari kubwa lakini hakuna kitisho dhidi yao kwa sasa. Abu Mohammed al-Golani, kamanda wa zamani wa kundi la Qaida aliyekata mafungamano yake na kundi hilo miaka mingi iliyopita anaongoza kundi kubwa la waasi nchini Syria na anatarajiwa kuhusika kutoa muelekeo wa mustakabali wa taifa hilo. 

Viongozi watoa hisia zao baada ya utawala wa Assad kuangushwa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture-alliance

Viongozi mbali mbali wa dunia wameendelea kutoa hisia zao, baada ya waasi Syria kutangaza kuuangusha utawala wa Bashar Al Assad. 

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, amesema kwa sasa Syria haitakiwi kuanguka katika mikono ya makundi mengine yaliyo na itikadi kali. Amehimiza ulinzi kamili wa makundi ya kidini na makabila ya wachache kama ya Wakurdi na Wakristo.

Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Angela Rayner, amesema kile kinachohitajika kwa sasa ni uthabiti wa kikanda akisema udikteta na ugaidi umesababisha madhila makubwa kwa watu wa Syria.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Geir Pedersen pia amezungumzia hali ya Syria na kusema ukurasa mpya umefunguliwa nchini humo na anatumai utakuwa wa amani, maridhiano, uadilifu na unaowajumuisha Wasyria wote. 

Rais wa Marekani Joe Biden kupitia msemaji wa usalama wa taifa Sean Savett, amesema Marekani inafuatilia matukio ya Syria kwa karibu, huku Ufaransa ikisema itaendelea kusimamia usalama wa kanda nzima na kuitakia Syria amani umoja na uhuru. China pia imesema inafuatilia kwa karibu hali nchini Syria. 

Vyanzo: afp/reuters/ap