1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyenusurika katika ajali ya ndege ya Yemenia awasili Ufaransa

Kabogo Grace Patricia2 Julai 2009

Abiria pekee aliyenusurika katika ajali ya ndege ya Yemenia iliyotokea Jumanne, awasili Ufaransa akitokea Comoro

Kassim Bakari, baba wa msichana Bahia Bakari, abiria pekee aliyenusurika katika ajali ya ndege ya Yemenia.Picha: AP

Abiria pekee aliyenusurika katika ajali ya ndege ya shirika la ndege la Yemen-YEMENIA, iliyotokea katika visiwa vya Comoro mwanzoni mwa juma hili, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Le Bourget karibu na mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Abiria huyo, msichana mwenye umri wa miaka 13 Bahiya Bakary, aliwasili nchini Ufaransa kwa ndege huku akiwa amesindikizwa na Naibu Waziri wa Maendeleo wa Ufaransa, Alain Joyandet.

Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Bahiya alilakiwa na baba yake mzazi, Kassim Bakary na jamaa wengine wa familia yake. Alipelekwa katika hospitali moja ya mjini Paris kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha aliyoyapata, ambayo ni pamoja na kuvunjika bega na majeraha ya moto.

Msichana huyo ambaye ni raia wa Ufaransa mwenye asili ya Comoro, alikaa kwenye maji kwa takriban saa 12 baada ya ndege hiyo kuanguka, huku abiria wengine walionusurika naye kufariki, kutokana na kushindwa kujiokoa. Kusalimika kwa msichana huyo ni sawa na maajabu kutokana na baba yake mzazi kusema kuwa mtoto wake huyo hajui kuogelea.

Kwa upande wake Waziri Joyandet amesema ameshangazwa na hali ya afya aliyonayo msichana huyo akisema inatia moyo. Ndege hiyo chapa ya Airbus A 310 ilikuwa imebeba abiria 142 na wafanyakazi 11, wakati ilipoanguka katika Bahari ya Hindi Jumanne kutokana na hali mbaya ya hewa.

Kati ya abiria hao, 75 walikuwa raia wa Comoro, 65 raia wa Ufaransa, raia mmoja wa Palestina na mmoja wa Canada.

Ndugu za marehemu wamesema kuwa ndege hiyo haikuwa salama hivyo, isingeruhusiwa kuruka na kwamba ndege hiyo ilizuiwa kuingia nchini Ufaransa mwaka 2007, baada ya wakaguzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Ufaransa, kubaini makosa kadhaa katika ndege hiyo.

Aidha, Mkuu wa kitengo cha ufundi cha Shirika la ndege la Yemenia, Hassan Al-Hauthi, amesema kuwa rubani wa ndege hiyo hakutoa taarifa wala ishara yoyote kama kulikuwa na matatizo ya kifundi katika ndege hiyo.

Kutokana na mkanganyiko uliopo juu ya ndege hiyo, Naibu Waziri wa Usafiri wa Ufaransa, Dominique Bussereau ametaka kutafutwa kwa mashirika ya ndege yanayorusha ndege zisizo salama.

Katika hatua nyingine, Rais wa Comoro, Ahmed Abdallah Sambi, leo amerejea nchini kwake baada ya kuahirisha safari yake ya Libya alikokuwa ahudhurie mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika, ulioanza jana. Kurejea kwa Rais Sambi ni kutokana na ajali hiyo ya ndege, na baada ya kuwasili rais huyo alikutana na maafisa wa serikali katika uwanja wa ndege wa Moroni, ambako pia alifanya mazungumzo na ndugu za watu waliokufa katika ajali hiyo.

Ndege ya Rais Sambi imekuwa ni ndege ya kwanza kutua katika uwanja wa Moroni, tangu kutokea kwa ajali hiyo ya ndege ya Yemenia. Hata hivyo, Rais Sambi hakuwa na mazungumzo yoyote na waandishi habari.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE/RTRE/)

Mhariri: M. Abdul-Rahman





Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW