Alonso amfagilia Jude Bellingham
26 Juni 2025
Siku ya Jumapili, Bellingham alifunga goli lake la kwanza akiwa chini ya Alonso, wakati Real Madrid ilipoilaza klabu ya Pachuca ya Mexico, kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu.
Manguli hao "Los Blancos" watamalizia mbio za makundi kwa kukipiga na RB Salzburg huko Philadelphia, na ikiwa watashinda watasonga mbele kwenye raundi ya 16 bora wakiwa vinara wa Kundi H.
Timu zote mbili zina pointi sawa baada ya michezo miwili, huku timu ya Al Hilal ya Saudi Arabia ikiwa na pointi 2.
"Ni wazi, ataendelea kuwa mchezaji muhimu kwetu," alisema Alonso alipomzungumzia Bellingham kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi. "Ninapenda anachofanya anapokuwa uwanjani na jinsi anavyojituma kwenye michezo yote.
"Ana ubora wa hali ya juu, tuliona alivyocheza dhidi ya Pachuca, na tupo karibu naye wakati wote. "Jude ana matamanio mengi, anataka kuimarika na kuendelea kukua, na tunataka kuendelea kuona jinsi anavyokua."
Kylian Mbappe ameachwa kwenye kikosi cha Real Madrid, licha ya kurejea kwenye mazoezi siku ya Jumatano baada ya kuugua.