1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alonso asema bado mapema mno kuzungumzia taji

5 Aprili 2024

Kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso amesisitiza Ijumaa (05.04.2024) kwamba ni mapema mno kuzungumzia taji la Bundesliga licha ya timu yake kuwa na mwanya wa alama 13 kileleni mwa Bundesliga.

Kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso
Kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi AlonsoPicha: Cathrin Müller/MIS/IMAGO

Leverkusen wanaweza kushinda taji lao la kwanza kabisa la Bundesliga mapema wiki ijayo, kutegemea na matokeo ya mabingwa watetezi Bayern Munich ambao wako katika nafasi ya pili.

"Katika soka chochote kinaweza kutokea," Alonso aliwaambia waandishi habari, akisema "bado ni mapema mno."

"Tuko katika nafasi nzuri sana. Lakini hatuzungumzii taji, tunazungumzia kuhusu mpinzani anayefuata."

Bayer Leverkusen wanakwaana na Union Berlin Jumamosi (06.04.2024) huku Bayern wakisafiri kucheza ugenini na Heidenheim iliyosimama katika nafasi ya 11. 

Kikosi cha kocha Alonso kinakaribia ufahari wa msimu wa mafanikio mazuri, baada ya pia kufuzu kwa fainali ya kombe la shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal, kufuatia ushindi wa 4-0 dhidi ya Fortuna Duesseldorf Jumatano, uliorefusha kutokushindwa kwao hadi mechi 40 msimu huu.

Alonso asema mashabiki wana stahamala

Raia huyo wa Uhispania, ambaye wiki iliyopita alisema alipania kuendelea kuwa kocha wa Leverkusen msimu ujao licha ya kunyatiwa na Liverpool na Bayern Munich, alisema sio tu kwamba wachezaji wanaelekeza nguvu kwa mechi inayofuata, bali pia mashabiki hawapiti mbele huku kukiwa na uwezekano wa kushinda mataji matatu msimu huu.

Mnamo 2002, Leverkusen walikuwa mbele katika ligi na walikuwa wamefuzu kwa fainali ya kombe la shirikisho na ligi ya mabingwa Ulaya, lakini wakapoteza mataji yote matatu.

"Mashabiki ni werevu na wanaweza kukumbuka kilichotokea wakati wa nyuma. Wana stahamala."

"Tunataka kusherehekea wakati tunapoweza kusherehekea. Na sasa sio wakati wa kusherehekea, ni wakati wa kufanya kazi na kujiandaa."

Soma pia: Alonso muda wa kusherehekea ushindi bado

Alonso alisema mshambuliaji Victor Boniface, ambaye amerejea baada ya kuuguza jeraha na kucheza kwa mara ya kwanza mwaka huu 2024 dhidi ya Duesseldorf siku ya Jumatano, ataanza katika kikosi cha kwanza Jumamosi.

"Anaweza kuanza mechi, lakini tumeamua kutomchezesha kuanzia mwanzo. Ilikuwa vizuri kwake kucheza dakika 25 au zaidi siku ya Jumatano. Tunataka tumsaidie arejee katika hali yake vizuri na ajihisi vizuri. Tunamhitaji."

(afpe)