1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alonso: Real Madrid itarudi imara msimu ujao

10 Julai 2025

Kocha mpya wa Real Madrid, Xabi Alonso, amesisitiza kuwa kibarua chake cha kuiongoza Madrid kinaanza sasa rasmi, kufuatia kichapo cha 4-0 dhidi ya Paris Saint-Germain kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu.

FIFA Club World Cup 2025 | Halbfinale | Paris Saint-Germain vs. Real Madrid | Zweikampf zwischen Luka Modric und Warren Zaire-Emery
Picha: Lee Smith/REUTERS

Alonso alichukua nafasi ya Carlo Ancelotti siku chache tu kabla ya mashindano ya Kombe la Dunia la Vilabu kuanza, bila kupata muda wa kutosha wa maandalizi ya kikosi chake. Alieleza kuwa huu ni mwanzo mpya wa kujenga timu imara na yenye mshikamano kuelekea msimu ujao.

"Kipindi kipya kinaanza, kuna nafasi nyingi za kujiimarisha, mambo mengi tunataka kufanya vizuri zaidi lakini leo tumeumia. Lazima tujitafakari. Hatukua na mchezo mzuri. Lakini hili litatusaidia siku za usoni kujifunza jinsi ya kujiendeleza, jinsi ya kusonga mbele ili tuweze kushindana kwa kiwango bora zaidi kuliko tulichokifanya leo."

Mchezo dhidi ya PSG ulikuwa mtihani mgumu kwa Madrid, mabao mawili ya kwanza yalitokana na makosa ya safu ya ulinzi ndani ya dakika tisa. Na kipindi cha kwanza PSG walikuwa mbele 3-0 na kuandikisha kipigo cha kwanza kwa Alonso tangu alipotua Madrid.

Dembele astahili Ballon d'Or

Achraf Hakimi na Ousmane Dembele wakisherehekea bao.Picha: Peter Cziborra/REUTERS

Kwa upande mwingine, kocha wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique, alifurahia ushindi wa timu yake na kueleza kuwa PSG ni timu yenye nguvu isiyozuilika msimu huu. Enrique alimmiminia sifa mchezaji wake Ousmane Dembele, ambaye amekuwa nyota msimu huu kwa kuonyesha kiwango cha hali ya juu licha ya kuanza mashindano haya akiwa na jeraha hivi karibuni. Enrique ameashiria kuwa Dembele anastahili kupata tuzo ya mchezaji bora duniani ya Ballon d'Or.

"Ningependa kusisitiza kwamba hii ni mechi ya kwanza ambapo mchezaji wetu bora, OusmaneDembele, yuko imara kiafya. Mechi ya kwanza katika Kombe la Dunia la Vilabu. Alipata jeraha akiwa na timu ya taifa na hatukuweza kufurahia uchezaji wake. Alikuwa akicheza kwa dakika chache hapo awali, ana uwezo wa kubadilisha mchezo, mtu anayeleta tofauti, na ni mchezaji wa kipekee. Ni mchezaji mzuri na ninatumai atakuwa fiti kwa ajili ya fainali."

Dembele alifunga bao la pili katika mchezo dhidi ya Real Madrid, likiwa bao lake la 35 katika mechi 52 alizochezea PSG katika mechi za mashindano yote tangu Agosti mwaka jana. Ushindi wa PSG umezidi kuimarisha rekodi yao ya kushinda mataji msimu huu; tayari wametwaa Ligue 1, Kombe la Ufaransa, na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.

PSG sasa ina miadi na Chelsea siku ya Jumapili katika fainali itakayochezwa ndani ya uga wa MetLife. Chelsea ilijikatia tiketi mapema wiki hii baada ya kuilaza klabu ya Brazil Fluminense mabao 2-0. Kocha wa Chelsea Enzo Maresca amesema ana matumaini kwamba kikosi chake kitazidi kuimarika.

Safari ya Chelsea kufika fainali ya mashindano Kombe la Vilabu imejiri baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye Ligi ya Premer, hivyo kujihakikishia kurejea kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na pia kubeba ubingwa wa Conference League.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW