1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amani haijapatikana katika rasi ya Korea

Isaac Gamba
9 Septemba 2018

Wakati Korea Kusini ikijaribu kuyatekeleza kwa vitendo mahusiano yaliyoboreshwa hivi karibuni  kati yake na Korea Kaskazini, bado matatizo ya zamani yanasalia kuwa changamoto katika nchi hizo mbili,

Korea-Gipfel 2018
Picha: Getty Images

Wakati Korea Kusini ikijaribu kuyatekeleza kwa vitendo mahusiano yaliyoboreshwa hivi karibuni  kati yake na Korea Kaskazini, bado matatizo ya zamani yanasalia kuwa changamoto katika nchi hizo mbili, anaandika Peter Sturm wa Frankfurter Allgemeine Zeitung.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika hivi karibuni, zaidi ya theluthi mbili ya Wajerumani wanahofu juu ya sera za Rais Donald Trump wa Marekani na ingekuwa vyema iwapo kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, naye angekuwa na mtazamo kama huo.

Kwa vyovyote vile, kiongozi huyo wa Korea Kaskazini haonekani kuwa na ushahidi wa kutosha  kumuonesha Rais Trump kuwa ameanza tayari mchakato wa kuondoa silaha za nyuklia. Hata hivyo, hali katika Rasi ya Korea inaonekana kutulia zaidi kuliko ilivyokuwa miezi michache iliyopita, ingawa kwa hakika hakuna kilichobadilika hadi sasa.

Korea Kusini inafanya kila inaloweza kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo mahusiano yaliyoboreshwa kati yake na Korea Kaskazini pamoja na Marekani huku Rais Moon Jae-in  akisema anafanya hivyo licha ya hofu iliyopo kisiasa pindi mageuzi yanayotarajiwa kati ya nchi hizo tatu kuhusiana na hatua ya kuondoa silaha za nyukilia katika Rasi ya Korea yatakapogonga mwamba.

Aidha wachambuzi wanasema  kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anataka kuvuruga mahusiano ya karibu kati ya Korea Kusini  na Marekani.

Kwa upande mwingine, zaidi ya masilahi ya kiusalama, Marekani ina maslahi mengine  zaidi  hasa linapokuja suala linalohusu Rasi ya Korea.

 

Kim Jong Un bado anahitaji silaha za nyukilia

Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Reuters/K. Lamarque

Ingawa Korea Kaskazini imekuwa ikizungumzia kuondoa silaha za nyukilia, lakini haiingii akilini iwapo Kim Jong Un anamanisha kwa dhati juu ya hatua hiyo tofauti, na Trump pamoja na sehemu kubwa ya ulimwengu wanavyofikiria.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anaamini kuwa anahitaji silaha za nyuklia ili kuizuia Marekani kutoanzisha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo, hatua inayoonesha kuwa hakuna mkataba wa amani utakaosainiwa  ambao utamtenganisha na mapenzi yake katika hilo.   

Hata hivyo, suala linalohusiana na silaha za nyuklia limeiongozea heshima Korea Kaskazini kiulimwengu, hasa baada ya majaribio ya makombora iliyoyafanya miaka ya hivi karinuni.

Hayo yote yanajiri mnamo wakati Kim Jong Un akiadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 tangu  taifa la Korea Kaskazini lilipoasisiwa huku swali ikiwa ni je hatua iliyofikiwa hadi sasa kuhusiana na mjadala wa kuondosha silaha za nyuklia itadumu?

Mwandishi: Isaac Gamba/DW

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW