Amani yaadhimishwa duniani, DRC bado yakumbwa na mizozo
21 Septemba 2026
Wameyasema hayo wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya amani leo (21.09.2026).Vurugu za mara kwa mara zinazofanywa na makundi yenye silaha, hususan vita kati ya waasi wa AFC/M23 na serikali ya Kongo, zimesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao. Wakati huo huo, ukosefu wa usalama unaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi katika baadhi ya vijiji.
Espérance ni mkimbizi kutoka kijiji cha Luntukulu. Baada ya kupokelewa na kuhifadhiwa na familia moja mjini Bukavu, nyumba aliyokuwa akiishi iliteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo. Sasa anasema hana tena matumaini ya kupata amani kupitia binadamu yeyote.
Hali ya usalama pia inaendelea kusababisha madhara makubwa ya kibinadamu. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano yanaendelea katika eneo la mashariki mwa nchi licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa. Umoja huo unasema wanawake na watoto ndio wanaobeba mzigo mkubwa zaidi wa athari za mgogoro huu.
Sadiki Malabar, Mkuu wa shirika la utetezi wa watoto la Golden Unity, anasikitika kwamba vita hivyo vimewaathiri watoto kwa kiwango kikubwa.
Mapigano bado yanaendelea
Hivi karibuni, Rais Félix Tshisekedi alitangaza kuwa mazungumzo yatakayohusisha pande mbalimbali yatafanyika katika siku zijazo, ingawa hayatawahusisha watu waliobeba silaha kinyume na Katiba ya Kongo. Jean-Moreau Tubibu, mtetezi wa haki za binadamu na amani mjini Bukavu, alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa kila upande ili kuhakikisha kupatikana kwa amani ya kudumu na inayowajumuisha wote.
Wakati huo huo, mapigano makali yameendelea tangu mwishoni mwa wiki iliyopita katika baadhi ya vijiji vilivyo karibu na eneo la Minembwe, katika jimbo la Kivu Kusini. Mapigano hayo yanahusisha jeshi la Kongo linaloungwa mkono na makundi ya Wazalendo dhidi ya waasi wa AFC/M23/Twirwaneho.
Kila upande unautuhumu mwingine kwa kuanzisha mashambulizi na kutumia ndege zisizo na rubani kulenga vijiji vya raia.