Amani ya mashariki ya kati, kujiuzulu kwa waziri mkuu wa Brandenburg
30 Julai 2013Chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani SPD kimepata pigo katika kampeni yake ya kumuondoa madarakani Kansela Angela Merkel, kufuatia kujiuzulu kwa waziri mkuu maarufu wa jimbo la Brandenburg Matthias Platzeck kutokana na sababu za kiafya. Kuhusu hatua yake hiyo, gazeti la Die Welt linaandika:
Ni hali ya kuhuzunisha kujiuzulu kwa mtu ambaye anaambatanisha kuondoka na kujiamini na vile vile kukata tamaa na kushindwa. Platzeck ndie mtu pekee kutoka mashariki mwa Ujerumani aliekiongoza chama cha SPD bila kuacha athari nyuma. Uongozi wake katika jimbo la Brandenburg utakumbukwa katika vitabu vya historia. Ingawa alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu, hakuacha kujihisi kama mtu wa nje. Kiongozi huyo tegemezi wakati wa mafuriko makubwa katika mto Oder mwaka 1997 hakuwa mwenye nguvu kama alivyoonekana. Ni kama vile alikuwa amewasili katika Jamhuri ya shirikisho akitokea Ujerumani mashariki, lakini hatimaye amepotea.
Wawakilishi wa Israel na Palestina wako mjini Washington, Marekani, kufanya maandalizi kwa ajili ya mazungumzo ya amani ya moja kwa moja. Lakini gazeti la Süddeutsche lina wasiwasi juu ya ufanisi wa mazungumzo hayo. Mhariri wa gazeti hilo anasema:
Bado haiko bayana iwapo mazungumzo mapya yanatokana na nia ya dhati ya pande mbili kufikia muafaka, au yanavisha kilemba cha ukoka majivuno ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani ya kutaka kuuwa dubwana la mchakato wa amani ya mashariki ya kati. Itakuwa vizuri kufahamu iwapo waziri John Kerry anafanya hivi kivyake au kwa niaba ya rais Barack Obama ambae alionyesha kukatishwa tamaa baada ya kushindwa kwa jaribio la awali kutanzua mgogoro huo. Je, Obama sasa amebadili mtazamo wake na atakuwa tayari kuingilia kati mwenyewe badala ya waziri wake wa mambo ya kigeni, na kuwalaazimisha Waisrael na Wapalestina kusaini makubaliano? Hilo hatujui.
Gazeti la Neue Osnabrücker pia linatathmini mpango huo wa kidiplomasia na linasema matumaini ya ufanisi ni madogo sana kwa kuzingatia vita vinavyoendelea nchini Syria, na machafuko ya kisiasa nchini Misri. Lakini Mhariri wa gazeti la Mittel Bayerische anaona ipo fursa na anasema:
Tofauti na hali ilivyo nchini Syria na Misri, Marekani inazo nyenzo inazoweza kutumia kwa ufanisi, kuzishawishi pande mbili. Israel inapenda kuhakikishiwa usalama wake na Wamarekani kutokana na mgogoro wa kinyuklia wa Iran, na pia inaiona Marekani kama nchi pekee inayoweza kuzuia utambuzi wa upande mmoja wa taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa. Wapalestina wanavutiwa na ahadi ya kuwa na taifa lao huru, ambalo jamii ya kimataifa imeahidi kulisaidia kwa msaada wa dola za marekani bilioni nne.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman